Kamati ya Mifugo, Kilimo na Uvuvi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imefanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa na Halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa Fedha 2023/2024 (Oktoba hadi Desemba 2023) ambapo leo tarehe 26 Februari, 2024 imetembelea mradi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti na kuridhishwa na maendeleo ya machinjio hiyo.
Akiongea wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Abdulkharimu Masamaki ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa Mradi huo ambao utakwenda kubadilisha maisha na uchumi wa watu.
"Nilipongeze Jiji la Dar es Salaam kwa kujenga machinjio hii ya kisasa. Mradi huu unakwenda kufungua fursa nzuri kwa Wafanyabiashara wa Vingunguti na Ilala kwa ujumla na mikoa mingine kwa sababu Dar es Salaam inategemewa sana katika soko la mifugo. Lakini pia utatoa fursa kwa wafanyabiashara kupeleka nyama nje ya nchi. Hivyo niwasihi viongozi kumsimamia kikamilifu Mkandarasi anaefanya Ujenzi wa Chumba cha kuhifadhi ubaridi (cold room) kumaliza kwa wakati ili machinjio iweze kuanza kufanya kazi rasmi." Amesema Mhe. Masamaki.
Mradi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti ulianza rasmi tarehe 8 Julai 2019 na unatekelezwa na Mkandarasi ambaye ni Shirika la nyumba la Taifa (NHC) akisimamiwa na Mshauri Mwenezi M/S CONS AFRIKA Ltd na FB Consultant wa Dar es Salaam.