DC Mpogolo awataka walimu wa mkataba kuzingatia nguzo za Utumishi wa Umma

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka walimu wa ajira za mkataba walioajiriwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuzingatia nguzo 5 za utendaji, na kuwa wazalendo kwa Nchi katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yao.



Hayo ameyasema Leo tarehe 16 Aprili, 2024 katika kikao kilichojumuisha Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na walimu wa ajira za mkataba katika Ukumbi wa Arnatoglou kwa lengo la kuwaasa na kuwaelekeza walimu wa mkataba yale wanayopaswa kwenda kuyafanya wakiwa kazini. 



Akiongea na walimu wa mkataba Mhe. Mpogolo amesema “Natoa pongezi kwa walimu walioajiriwa na Halmashauri yetu, nawaasa muitumie nafasi hii mliyoipata kwa kuishi katika nguzo 5 ambazo ni kujua jukumu lako kwa watoto, kujifunza kuishi na kuendana na jumuiya inayokuzunguka, kujua mwajiri wako anataka nini, kujua jukumu lako kama mwalimu, na kujua wajibu kwa Taifa lako. Pia nawaomba mkaongeze juhudi na bidii katika ufundishaji ili kupandisha ufaulu katika shule ili Jiji letu liendelee kuwa kinara katika Elimu."

Aidha, Akiongea katika kikao kazi hicho Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwa jitihada anazozifanya za kuboresha Elimu katika Jiji la Dar es Salaam huku akimuhakikishia kutekeleza yale yote aliyoyaagiza.



Naye, Kaimu Afisa Elimu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Doreen Masawe ameeleza kuwa “Nipende kumshukuru Mkurugenzi wa Jiji kwa kuajiri walimu 150 wa mkataba katika masomo ya sayansi kwani kutokana na ajira hizo changamoto ya ufaulu katika masomo ya sayansi itakua imetatuliwa kwa kiasi hivyo Nipende kuwahakikishia kupitia ajira hizi ufaulu utazidi kuongezeka zaidi katika Halmashauri yetu."



Aidha, akimwakilisha Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Fidea Mapunda amewakumbusha walimu wajibu wao katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu kwa kutimiza majukumu yote ya kitaifa na kijamii kwa kuwalea watoto kwa maadili ya kinidhamu pamoja na kuzingatia sheria na kanuni za Utumishi wa Umma ikiwemo utoaji wa huduma Bora bila upendeleo, pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kwa wakati katika ubora unaotakiwa kwani walimu ndio kioo cha maadili nchini ambapo kwa kuzingatia hayo sekta ya Elimu nchini itazidi kuimarika.



Akiongea kwa niaba ya Afisa udhibiti ubora wa Shule Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Pudensiana Justine Kisela abeles kuwa “Kikao hichi ni muhimu sana kwenu katika kuhakikisha sekta ya elimu katika Halmashauri yetu inakua kwa kasi hivyo niwaase Waalimu muwe wabunifu kuwajengea wanafunzi uwezo mkubwa wa kufikiri na sio kukariri tu kwaajili ya mitihani. Pamoja na hayo nitoe wito kwa Wakuu wa Shule kuhakikisha mnasimamia walimu wengine kutumia zana za kazi pamoja na kuandaa azimio la kazi Ili kuandaa andalio la somo kama Wizara inavyoelekeza lengo likiwa ni kuleta wepesi wakati wa kufundisha."

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi