Kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, Jiji la DSM lapanda miti 150 Zahanati ya Kinyerezi

Katika kuelekea Sherehe za Kilele Cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, Viongozi na Wananchi wa Kata ya Kinyerezi leo Aprili 18, 2024 wamejitokeza kupanda miti takribani 150 katika Zahanati ya Kinyerezi lengo ikiwa ni kuendeleza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira.


Akiongoza zoezi hilo la upandaji wa miti, Mkuu wa Kitengo Cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Theresia Denis amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu ambapo wanatarajia kupanda miti katika kata zote 36 za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni kutekeleza muongozo wa Serikali wa kusherekea miaka 60 ya Muungano kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.


Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Muongozo huo wa Uhifadhi wa Mazingira na amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogogo kwa kuwa kinara wa Utunzaji wa Mazingira na kuahidi kuendelea kuyatunza kwa ajili ya Afya bora ya wananchi na Mazingira kwa ujumla.


Sambamba na hayo, ametoa Rai kwa wananchi kuwa na tabia ya kupanda miti kwa wingi na kuitunza kwa kuzingatia faida zinazotokana na miti hiyo.


Kwa upande wake Mkuu wa Kanda Namba nne Ndg. Siraji Ngarambe amewashukuru viongozi na wananchi wote waliojitokeza katika zoezi hilo la upandaji wa miti na kusema kuwa yeye Kama Kiongozi wa Kanda hiyo atakuwa mstari wa mbele katika kuitunza vyema ili malengo makuu la Serikali ya uanzishwaji wa kampeni ya upandaji miti hiyo yaweze kufikiwa.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi