Afisa Lishe Jiji la DSM ahimiza uzingatiaji wa lishe bora kwa mama wajawazito

Afisa Lishe wa Jiji la DSM Bi. Neema Mwakasege amewataka mama wajawazito kuzingatia lishe bora kwani lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu kwasababu humpatia mama virutubishi muhimu kulingana na hali yake. Wakati wa ujauzito mama anahitaji virutubishi zaidi kwa ajili ya maendeleo yake kiafya pamoja na mtoto aliyetumboni. Lishe bora huimarisha afya ya mama na humsaidia mtoto kukuwa vizuri kimwili na kiakili.


Bi. Mwakasege ametoa wito huo leo Juni 21, 2024 wakati wa muendelezo wa kampeni ya uhamasishaji lishe bora kwa mama wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano iliyofanyika katika Zahanati ya Kiwalani Jijini Dar ee Salaam Sambamba na kaulimbiu isemayo ‘Lishe bora kwa baba, mama na mtoto ni msingi wa jamii bora na Taifa endelevu’.


Akiongea katika hafla hiyo Bi. Mwakasege amesema “Lishe ni muhimu katika suala zima la ukuaji wa watoto. Lakini pia nitoe wito kwa kwa akina baba kushiriki katika kupambania masuala ya lishe kwa watoto wenu kwani Sisi kama Serikali tumeweka mikakati ya kuhakikisha wazazi na walezi wanazingatia lishe bora hii ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha jamii zetu zinazingatia afua za lishe."


Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kiwalani Dkt. Neema Mtobesya ameeleza kuwa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii imeendelea kutekeleza maagizo ya kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa na lishe inazingatiwa kwa kufanya semina mbalimbali kuhusu lishe kwa mama wajawazito, wababa na watoto chini ya umri wa miaka mitano.


Ikumbukwe kuwa ajenda hii ya lishe ni moja kati ya mipango endelevu ndani ya Jiji la Dar Es Salaam na Taifa kwa ujumla hivyo ni muhimu kila mwananchi kuzingatia lishe bora kwa Ustawi wa Jamii.





Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi