DC Mpogolo alipongeza Jiji la DSM kwa kuimarisha Sekta ya Afya

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Pongezi hizo amezitoa leo Juni 28, 2024 wakati wa Hafla ya ugawaji vifaa tiba kwa Idara ya Afya iliyofanyika katika ukumbi wa Arnatoglou Jijini humo.


Akikabidhi vifaa hivyo Mhe Mpogolo amesema “Napenda kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ukusanyaji wa mapato zaidi ya bilioni 100 ambapo wameweza kuvuka lengo la kukusanya bilioni 89 kwani kupitia fedha hizi wameweza kununua vifaa tiba vya shiingi Bilioni 1.6 huku zaidi ya milioni miatatu zikitumika kununua vifaa vya TEHAMA na Milioni 11 zikitumika kukata bima za ICHF kwa watoa huduma za afya ngazi ya Jamii hivyo kutokana na vifaa hivi huduma za afya zinaendelea kuboreshwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na hii inaonesha jinsi gani Jiji la Dar es Salaam linatimiza adhma ya Mheshimiwa Rais WaJamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa na zinawafikia wananchi kwa wakati.”


Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo aliweza kukabidhi vyeti vya mafunzo kwa timu za usimamizi vituoni (HMT’S 164) pamoja na bima za afya 277 kwa watoa huduma ngazi ya jamii huku akiwataka watoa huduma za jamii ngazi ya afya kuwa waadilifu kwa kuhakikisha wanazingatia utoaji wa huduma bora kwa wananchi pamoja na kutoa wito kwa viongozi waliopatiwa vyeti vya mafunzo kuhakikisha wanajali wananchi wanaowahudumia bila kusahau kubainisha changamoto za afya zilizopo ngazi ya jamii ili zipatiwe ufumbuzi.

Baadhi ya vifaa tiba vilivyogharimu jumla ya shilingi bilioni 1.6 ambavyo vitagawiwa kwa Zahanati na Vituo vya Afya kwaajili ya kuimarisha huduma za afya 

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto ameeleza kuwa Jiji la Dar es Salaam limepata bahati ya kupata fedha nyingi kutoka Serikali Kuu ambazo zinatumika kwenye Miradi ya Afya , Elimu na kuboresha miundombinu ya afya hivyo kutokana na ukusanyaji mkubwa wa mapato Jiji la Dar es Salaam limeweza kununua vifaa tiba ili kuhakikisha huduma za afya katika Jiji hilo zinaimarika kwa kasi.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto akiongea wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa tiba hivyo

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomaary Satura ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya huku alieleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mapato yake ya ndani inaenda kutekeleza ujenzi wa hospitali kubwa tatu zitakazoenda kupunguza changamoto ya msongamano wa wagonjwa pamoja na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati.

Mmoja wa watoa huduma ngazi ya jamii akipokea kadi ya bima ya afya jamii iliyoboresha (iCHF)

Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Jiji la Dar es Salaam Dkt. Zaituni Hamza ameeleza kuwa “Katika kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa jamii, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Afya ilipanga kununua vifaa tiba mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 vya jumla ya shilingi bilioni 1.6 ikiwa ni fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na Serikali kuu ambapo leo tumeweza kukabidhiwa Ultra Sound 15 pamoja na vifaa vya TEHAMA ambavyo vinaenda kuleta mabadiliko katika sekta afya kwenye Jiji letu hivyo tunaahidi kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili wananchi waweze kupata huduma bora kwa wakati.”


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi