Tanga Pharmaceutical and Plastic Ltd watoa Madawati 25 katika Shule ya Msingi Vingunguti

Wafadhili kutokaTanga Pharmaceutical and Plastics Limited (TPPL) leo tarehe 23 Machi, 2023 wametoa msaada wa madawati 25 kwa Shule ya Msingi Vingunguti iliyopo Kata ya Vingunguti ikiwa ni sehemu ya mchango wa wadau wa elimu kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma katika mazingira bora na tulivu.


Akiongea katika hafla hiyo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto aliwashukuru wadau hao kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu nchini huku akiwaahidi kuendelea kushirikiana nao katika kujenga na kuimarisha sekta ya elimu nchini

Halmashauri iko tayari kushirikiana na wadau wa maendeleo na nitahakikisha kuwa yote ambayo ni muhimu zaidi yatatekelezwa kwa wakati. Nawashukuru sana wadau kwa kuweza kuwa sehemu ya kuipa kipaumbele elimu Kwani Tanga Pharmaceutical and Plastic Ltd wamekuwa wadau wazuri sana katika kuchangia maendeleo ya Elimu katika Halmashauri yetu kwani leo hii wametoa madawati 25 kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Vingunguti huku mwaka 2020 waliweza kuchangia Friji Saba katika Kata ya Vingunguti ambazo zinasaidia katika Shule zetu na Zahanati yetu ya Vingunguti , Kwa hakika nyie ni marafiki wa kweli wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hatuwezi kuwalipa”.


Sambamba na hilo Mhe.Kumbilamoto aliweza kumkabidhi Cheti cha shukrani Meneja kutoka Tanga Pharmaceutical and Plastic Ltd ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kuunga mkono sekta ya elimu katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Aidha Mhe. Kumbilamoto ametoa wito kwa wazazi na walezi wa watoto wa Shule ya Msingi Vingunguti kuchangia fedha ya chakula kwa watoto wetu kwani Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekua akijitoa sana katika kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika hivyo kwa kutambua juhudi hizo wazazi wanahitaji nao kuchangia fedha kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi ili waweze kusoma kwa bidii wakiwa na afya njema.

Akikabidhi madawati kwa niaba ya wadau hao Meneja Muajiri kutoka Tanga Pharmaceutical Ltd Ndg. Stephen Godfrey amesema “Nina furaha sana kwa kampuni yetu kuwa miongoni mwa wadau wa maendeleo katika kukuza sekta ya elimu nchini hivyo nipende kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuchochea maendeleo katika sekta ya elimu kwani juhudi zake zote ndio zimefanya leo hii sisi kuchangia madawati 25 katika shule ya Vingunguti hivyo niwaombe wanafunzi kusoma kwa bidii ili kukuza ufaulu katika Halmashauri yetu ya Jiji la Dar es Salaam.


Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Vingunguti Mwl. Mfaume Fadhili amesema “Tunaishukuru sana kampuni ya Tanga Pharmaceutical and Plastic Ltd kwa kuwa mdau wetu mzuri wa maendeleo katika kukuza sekta ya elimu kwani hii leo tunafuraha kupata madawati haya 25 ambapo kwa kiwango chake tumendelea kupunguza idadi ya uhitaji wa madawati katika shule hii ya Msingi Vingunguti yenye jumla ya wanafunzi 2514. Pia tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya miaka hii miwili ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu kwani tuliweza kupata madawati 50."

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi