Katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo Septemba 06, 2024 Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala imepokea Taarifa ya Utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia Januari - Juni 2023.
Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Arnatouglou Jijini DSM na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala, Mkuu wa Wilaya wa hiyo, Wajumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya ya Ilala pamoja na Watumishi kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala Ndg. Alhaji Said Sidde amesema “Niwapongeze Wajumbe wa Halmashauri Kuu kwa kupokea na kupitisha Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia nipende kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kutekeleza Ilani ya Chama kwani wameweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuboresha huduma za wananchi. Niwaombe viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha mnatekeleza yale yote tuliyowaelekeza wakati wa ziara yetu na pia muhakikishe miradi yote inatekelezwa kwa wakati uliopangwa pia niwaombe wajumbe kuhakikisha mnashiriki kikamilifu kujiandikisha kupiga kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024."
Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa katika kuimarisha hali ya ulinzi na usalama Wilaya inaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Ilala kwa kuhakikisha Ilala ipo Shwari.
Aidha Mhe. Mpogolo ameendelea kusema “Katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Idara zake zikiwemo Idara ya Elimu, Idara ya Afya pamoja na Idara ya Maendeleo ya Jamii ambapo katika Idara ya Elimu Msingi na Sekondari, Halmashauri ya Jiji la DSM imeendelea kuboresha miundombinu ya shule za msingi kwa kipindi cha miaka minne ambapo zaidi ya bilioni 7 fedha kutoka mradi wa Boost, EP4R na mapato ya ndani ya Halmashauri zikitolewa kutekeleza miradi ya ujenzi wa madarasa Elimu msingi pamoja na uboreshaji wa miundombinu huku kwa upande wa Elimu Sekondari kwa kipindi cha miaka minne Halmashauri imeweza kujenga shule nane za ghorofa zikiwa na madarasa 20 pamoja na matundu 45 ya vyoo ambazo zimekua chachu ya kupunguza msongamano wa wanafunzi mashuleni huku Halmashauri ikiwa na mkakati wa kujenga maghorofa mengine 10 ya namna hiyohiyo,utekelezaji wa wa miradi hii umetokana na fedha kutoka Gharama za mpango wa Elimu bila malipo, Serikali Kuu, Mapato ya Ndani ya Halmashauri na wafadhili, SEQUIP na BARRICK. Pia miundombinu ya Afya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka minne imepokea kiasi cha zaidi ya bilioni 100 zikiwa ni za ukarabati wa miundombinu chakavu, Ujenzi wa vituo tisa vya Afya ambapo vituo saba vimekamilika na vituo viwili vikiwa katika hatua za mwisho, ujenzi wa hospital na ununuzi wa vifaa tiba ikiwemo mashine za kisasa halikadhalika idara hiyo imepokea magari ya kubebea wagonjwa takribani 6, magari manne yakiwa yamepokelewa kutoka Serikali kuu na magari mawili yakinunuliwa kwa fedha za mapato ya ndani hivyo kuleta jumla ya magari 12 ya kubebea wagonjwa. Kwa upande wa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imefanya uhamasishaji na kutoa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambapo Halmashauri imeweza kutoa kiasi cha Tsh bilion 17. 2 kwa vikundi 1462 aidha idara hiyo imeweza kuwatambua vijana elfu 12 wa bodaboda lengo likiwa ni kuhakikisha wanatambua vituo vyao ili vijana hao wa Bodaboda waweze kuvaa vazi rasmi na pindi fursa za mkopo wa asilimia 10% vijana hao waweze kupata, vilevile idara hiyo imeendelea kuunga mkono matumizi ya Nishati safi ya kupikia ambapo zaid ya mama lishe elfu moja wametambuliwa na baadhi yao wameweza kupewa majiko.”
Katika hatua nyingine, Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweka mipango endelevu ya kujenga masoko ya kisasa yatakayowasaidia wananchi kujipatia kipato na Jiji kuendelea kupata mapato
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo ameendelea kusema “Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Wilaya ya Ilala, pia ameweza kuishukuru Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya kwa kushirikiana na Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha tunatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi hivyo nikuahidi miradi mingine ambayo haijakamilika inaenda kukamilika kwa wakati na pia nikuhakikishie tutaenda kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wananchi kwa kuhakikisha wanafahamu maendeleo yaliyofanyika na serikali yetu kwa miaka mitano pia nikuhakikishie kwenda kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujiandikisha na kushiriki kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27,Novemba 2024”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndg. Elihuruma Mabelya ameeleza kuwa “Nipende kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za utekelezaji wa miradi kwa Halmashauri yetu kwani Sisi kama Halmashauri mipango yetu inaongozwa na Ilani ya CCM katika yale yote tunayoyatekeleza kwenye Kata na mitaa yetu kama uboreshaji wa miundo mbinu mbalimbali ya Afya , elimu na barabara hivyo niombe ushirikiano wenu kama Halmashauri Kuu ya Wilaya kuhakikisha Ilani ya Chama inatekelezwa katika Halmashauri yetu na nipo tayari kupokea maelekezo nitakayopewa”.