kamati ya mipango miji na mazingira yafanya ziara katika maeneo mbalimbali


  •        lengo ni kubaini barabara na madaraja yaliyoathirika na mvua zinazoendelea       
  •    maagunia aina ya kisalfet yaliyojazwa michanga yasaidia kutengeneza vivuko vya dharura 

  Na: Lucy Semindu Ilala

Kamati ya mipango miji na mazingira ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jana ilifanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Ilala kubaini barabara zilizoathirika na mvua.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira Mhe. Sultan Salim aliiongoza kamati yake katika maeneo hayo. Kata ziizotembelewa ni Kata za Chanika,Pugu ,Majohe ,Gongo la mboto, Ukonga, Kivule na Kata ya Kitunda.

Katika Kata ya Majohe Diwani wa Kata hiyo Mhe. Green Chilambo aliwaongoza wajumbe wa Kamati ya Mipango miji katika maeneo mbalimbali ya Kata yake. Mhe. Chilambo aliieleza kamati kuwa katika Mtaa wa Kichangani watu watatu walifariki dunia baada ya nyumba yao kujaa maji wakati wakiwa wamelala.

 Pia alisema kuwa katika Kivuko cha kwa Edward ambacho kinaunganisha Kigogo fresh na eneo la Shule ya Msingi na Zahanti ya Majohe, mama mmoja kwa bahati mbaya alishindwa kuokoa mtoto wake mdogo ambaye alikufa baada ya kuchukuliwa na maji.

Maeneo mengine yaliyoathirika katika Kata hiyo ni Mtaa wa Kichangani kwa Ngozoma eneo la kwa Mzee Piro ambapo Nyumba 200 zimezungukwa na maji, barabara ya  Msongola mpaka Mtumbo,     Mfereji  kwa Dihoma ambao umekatika  na  kuachanisha barabara inayotoka Pugu Sekondari kuelekea Majohe na pia  kipande cha barabara kinachotoka Pugu Sekondari hadi Reli ya Tazara kuelekea Majohe kimeharibika.

Aidha, Kamati hiyo ilishuhudia jinsi mvua kubwa zilizonyesha mwezi huu zilivyoharibu barabara, madaraja, vivuko na mifereji. Katika Kata ya Chanika barabara iliyounganisha Taliani na Vikongoro ilikuwa imeaharibika sana kwani wakazi wa maeneo hayo imekuwa vigumu kuwasiliana kutokana na jinsi barabara hizo zilivyoharibika.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Vikongoro  Bw Seif Mwera, aliieleza kamati kuwa nyakati za mvua imekuwa vugumu hasa kwa wagonjwa kuweza kupelekwa kwenye zahanati kwani kuharibika kwa barabara  kimekuwa kikwazo kwa wananchi wa eneo hilo kupata huduma muhimu.

Nalo Daraja la Kimwani linalounganisha Msumbiji na Nzasa lilikuwa limevunjika. Mkazi wa eneo hilo Bi Mwajuma Shabani alisema kuwa imekuwa vigumu kupata mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa kuwa maeneo hayo hayafikiki kirahisi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chanika Mhe. Abdilahi Mpate ameeleza kuwa tathmini iliyofanyika imeonesha Kata yake imeathitika sana na mvua zinazoendelea kunyesha na kwamba ipo haya hatua za haraka zichukuliwe ili kurudisha mawasilano kati ya maeneo mbalimbali ya Kata yake.

Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Mhe. Jerry Silaa ambaye ni Diwani wa Kata ya Gongo la Mboto aliionyesha kamati ya mipango miji jinsi Kata yake ilivyoathirika na mvua hizo. Maeneo yaliyoathirika sana katika Kata hiyo ni, Daraja la Kiltex ambapo tuta la barabara limeondoka na  barabara nzima inayoelekea kiltex imeharibika vibaya.

Kamati pia ilikagua katika Kata ya Ukonga na kubaini barabara mbalimbali za Kata hiyo jinsi zilivyoharibika vibaya. Maeneo yaliyoathirika sana ni barabara iendayo Ulongoni.

Aidha kamati hiyo ilikagua barabara za Kata ya Kivule ambapo Diwani wa Kata hiyo Mhe. Nyansika Motena aliionyesha kamati ya mipango miji jinsi daraja la Kivule lilivyokatika.  Hata hivyo ilionekana jinsi wakazi wa eneo hilo walivyojaza mifuko ya aina ya kisalfet mishanga na kutengeneza kivuko cha dharula ambacho kimesaidia kuunganisha wakazi wa eneo hilo na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam. 

Eneo la Mwisho kutembelewa lilikuwa ni Kata ya Kitunda ambapo Mhe.  Mwalimu Daniel aliwaongoza wajumbe wa Kamati ya Mipango miji. Barabara zilizoonekana zimeharibika vibaya ni Darala la Magole, eneo la Pemba beach ambapo makazi ya watu yamezingirwa na maji na barabara ya Nyantira -Kipera ambayo imejaa mashimo makubwa.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kupitia Kamati ya Mipango miji na mazingira imekuwa katika shughuli zake za kila siku ikijitahidi kupanga na kusimamia utekelezaji wa   miradi mbalimbali ya barabara, madaraja na vivuko ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa kiwango kikubwa ili mawasiliano na usafiri  katika Manispaa ya Ilala yawezwe kuboreshwa.

Kuharibika kwa barabara kulikotokana na athari za mvua ni changamoto kubwa kwa kamati hiyo.  Ziara ya Kamati ya Kamati ya mipango miji na mazingira inaendelea leo katika Kata nyingine zilizoathirika na mvua.           

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi