BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA LAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 249.8 KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017


Na: Hashim Jumbe
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilala lililofanyika tarehe 02 Aprili, 2016 limepitisha Bajeti ya Halmashauri ya Shilingi Bilioni 249.8 kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 34 ikilinganishwa na  Bajeti ya mwaka wa fedha uliopita wa 2015/2016 ambapo Bajeti hiyo ilikuwa ni Shilingi Bilioni 164.06

Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ilala inatarajia kutumia jumla ya  Shilingi Bilioni 249.8 kwa shughuli za maendeleo na uendeshaji Taasisi, kati ya hizo Shilingi Bilioni 85.2 ni kutoka kwenye mapato ya ndani ‘own source’ ikiwa ni ongezeko la asilimia 34.4 ukilinganisha na makusanyo ya mwaka wa fedha uliopita wa 2015/2016 amabayo ilikuwa Shilingi Bilioni 55.8. Mchango wa fedha ya Ruzuku inayotarajiwa kutoka Serikali Kuu ni Shilingi Bilioni 164.6 nao ikiwa ni ongezeko la asilimia 31.7 ukilinganisha na mchango wa mwaka 2015/2016 wa Shilingi Bilioni 108.2

Awali kabla ya kikao cha Baraza, makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti ya mwaka 2016/2017 yalijadiliwa katika Kamati za kudumu za Fedha na Utawala, Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii, Kamati ya Mipango Miji na Mazingira na Kamati ya kudhibiti maambukizi ya Ukimwi. Baraza liliidhinisha Shilingi Bilioni 97.995 kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi, Shilingi Bilioni 41.847 ni kwa ajili ya matumizi Mengineyo, Shilingi Bilioni 2.428 ni kwa ajili ya Mfuko wa Pamoja wa Afya ‘Basket Fund’, na Shilingi Bilioni 107.538 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Mhe. Charles Kuyeko akifungua kikao cha Baraza la Madiwani, kikao hicho kilikuwa maalum kwaajili ya kuipitisha Bajeti ya Manispaa ya Ilala kwa mwaka wa fedha 2016/2017
Madiwani wa Manispaa ya Ilala pamoja na Watendaji wakiwa wamesimama wakati wa dua ya kukiombea kikao cha Baraza la Madiwani.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala aliyesimama akisoma taarifa ya makadirio ya mpango wa bajeti ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa mwaka wa fedha 2016/2017

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi