MANISPAA YA ILALA YAADHIMISHA SIKU YA MALARIA DUNIANI KWA KUTOA HUDUMA YA UPIMAJI MALARIA BURE KWA WANAFUNZI

Na: Hashim Jumbe
Hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa Wakazi wa Manispaa ya Ilala imezidi kupungua kwa asilimia 6.9, kutoka Wagonjwa  152,714 walioripotiwa kwenye vituo vya tiba vya Serikali na Binafsi kwa mwaka 2014 ukilinganisha na idadi ya Wagonjwa  142,099 kwa mwaka 2015.

Pamoja na kupungua kwa idadi kubwa ya Wagonjwa wanaoripotiwa kwenye vituo vya tiba vya Serikali na Binafsi bado Malaria ni tatizo kubwa kwenye Jamii ya Wakazi wa Manispaa ya Ilala.

Akiongea wakati wa maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya michezo vya Jakaya Kikwete  kwa Manispaa ya Ilala, Bwana Ally Adnani ambaye ni Mratibu wa Malaria Manispaa ya Ilala ameelezea mikakati  inayotekelezwa na Manispaa ya Ilala ili kuendelea kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa Wakazi wa Manispaa ya Ilala.

Bwana Adnani alisema “kwanza tumefanya utambuzi wa Wagonjwa, tiba sahihi ya Wagonjwa na ya tahadhari, pili tumefanya uhamasishaji, uelimishaji Jamii na utetezi kuhusu ugonjwa wa Malaria na tatu tumefanya uthibiti wa mbu waenezao malaria kwa njia ya utangamano, kama vile matumizi ya vyandarua  vyenye viuatilifu vya muda mrefu, kuua viluwiluwi wa mbu na usimamizi wa mazingira kwa kuondoa mazalio ya mbu.

Aidha, katika maadhimisho hayo, Manispaa ya Ilala imetoa elimu ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria na namna ya kujikinga kwake, na pia huduma ya upimaji bure wa ugonjwa wa Malaria kwa Wanafunzi wa shule za Msingi na za Sekondari zilizopo Manispaa ya Ilala zilifanyika kwenye viwanja hivyo vya michezo vya Jakaya Kikwete



Mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya Msingi Scholastica akifanyiwa vipimo vya ugonjwa wa Malaria.


Bwana Gharib Shomary akiwafundisha Wanafunzi wa shule ya sekondari Jamhuri namna viluwiluwi vinavyozalisha mbu



Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi