DC-MJEMA AFANYA UZINDUZI WA BODI NA KAMATI MPYA ZA HUDUMA ZA AFYA KWA MANISPAA YA ILALA

Na: Hashim Jumbe
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema, leo tarehe 28 Aprili, 2017 amefanya uzinduzi wa Bodi na Kamati mpya zitakazoshiriki katika uendeshaji na usimamizi wa utoaji huduma za afya katika vituo vya afya vinavyosimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Uzinduzi huo wa Bodi na Kamati za huduma za afya ni matokeo ya mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji wa huduma za afya yaliyoanza mwaka 1993/1994 yanayolenga kuhamasisha Jamii kumiliki huduma za afya na kuiwezesha Jamii kupanga, kuendesha, kusimamia na kutathmini utoaji wa huduma za afya katika Jamii.

Akiongea na Wajumbe wa Bodi na Kamati za huduma za afya wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mjema alisema “kuundwa kwa Bodi na Kamati za huduma za afya katika vituo vya tiba ni fursa muhimu katika kuendelea kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa mkakati wa huduma za afya ya msingi katika Wilaya yetu kwa kushirikisha Jamii”.

Naye, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Bi. Victorina Ludovick awali aliwasilisha taarifa inayoonesha  mafanikio ya uanzishwaji wa Bodi na Kamati za huduma za afya kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2010-2016, ambapo Mganga Mkuu alisema “uanzishwaji wa Bodi na Kamati za huduma za afya umefanikisha mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufanikisha suala la kupunguza vifo vya Mama wajawazito kutoka vifo 37 mwaka 2010 hadi vifo 19 mwaka 2016, vifo vya Watoto wachanga navyo vimepungua kutoka 309 kwa mwaka 2012 hadi vifo 205 mwaka 2016”.

Aidha, Bi. Victorina aliendelea kueleza mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na kuanzishwa kwa Bodi na Kamati za afya kuwa ni kuongezeka kwa fedha za uchangiaji kutoka Tsh. 50,000/= kwa mwezi mwaka 2006 hadi Tsh. 600,000/= kwa mwezi mwaka 2016 katika vituo vidogo na Tsh.  2,900,000/= hadi Tsh. 15,000,000/= kwa vituo vikubwa.
                                                                                 








Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi