DC-MJEMA AUNGANA NA WANANCHI WA KATA YA MAJOHE KUADHIMISHA SIKU YA MUUNGANO KWA KUSIKILIZA KERO MBALIMBALI NA KISHA AZINDUA UJENZI WA BARABARA YA PUGU-MAJOHE

Na: Hashim Jumbe

Tarehe 26 Aprili ya kila mwaka ni siku muhimu katika historia ya Watanzania, ni siku iliyozaliwa Taifa jipya kutokea kwenye Muungano wa Nchi mbili zenye historia inayofanana, Nchi ya Tanganyika na Zanzibar, ambapo mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar  na kuzaliwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’, hata hivyo jina hilo lilikuja kubadilishwa mano tarehe 28 Oktoba, 1964 na kuitwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.

Siku ya leo, Muungano huo unapofikisha miaka 53 tangu uasisiwe, Mkuu wa Wilaya ya  Ilala, Mhe. Sophia Mjema ameitumia siku ya leo kutembelea Kata ya Majohe na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili Wananchi wa maeno hayo, huku kero kubwa ikiwa ni kutiririka kwa maji machafu yanayotoka kwenye dampo la Kinyamwezi pamoja na harufu mbaya kutokea kwenye dampo hilo inayosambaa kwenye makazi ya Wananchi.

Aidha, Mbali na kero hiyo, Mkuu wa Wilaya pia alipokea kero ya miundombinu mibovu ya barabara kwa Wakazi hao wa Majohe, ambapo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha zimeleta adha kwa Wakazi hao na kukosa mawasiliano ya barabara zinazowaunganisha na kata za jirani, huku changamoto kubwa ya kuharibika barabara hizo ikiwa ujenzi holela wa makazi ya Wananchi hao.

Kero hizo mbili kubwa zilimlazimu Mkuu huyo wa Wilaya kumuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kutafuta ufumbuzi wa haraka wa namna ya kuzuia kutiririka kwa maji machafu kutoka kwenye dampo la Kinyamwezi kwenda kwa Wakazi wa maeneo hayo ya pemmbeni.

Mhe. Mjema pia alipiga marufuku ujenzi kwenye maeneo ya vyanzo vya njia za maji, huku akiagiza kwa Wananchi waliojenga kwenye maeneo hayo kubomoa haraka nyumba zao na Serikali haitowalipa fidia kwani maeneo hayo hayaruhusiwi kwaujenzi wa aina yoyote.

Mwisho, Mkuu wa Wilaya ya Ilala alizindua rasmi ujenzi wa barabara ya kutoka Pugu hadi Majohe yenye urefu wa Kilomita 7 inayojengwa kwa kiwango cha changarawe. Ujenzi wa barabara hiyo utachukua siku takribani 90 kuanzia leo siku ya uzinduzi.
                                                                                                                    












Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi