RC-MAKONDA ATOA MAAGIZO 17 KWA WATENDAJI WA IDARA YA ARDHI NA MIPANGO MIJI KWA HALMASHAURI ZA DSM

Na: Hashim Jumbe

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda leo ametoa maagizo 17 kwa Watendaji wa Idara ya Ardhi na Mipangomiji wa Halmashauri za Dar es Salam wakati wa kikao kazi cha kujadili changamato mbalimbali zinazoikumba sekta ya Ardhi ikiwa ni pamoja na migogoro isiyokwisha ya umiliki wa ardhi.

Katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Arnatouglou, Mhe. Makonda alitoa maagizo yafuatayo;

  1. Nisingependa kuona Mwananchi anakuja kwa Mkuu wa Mkoa kulalamika wakati Mkuu wa Idara upo na ungeweza kumsaidia matatizo yake.
  2. Kuanzia Juni nataka vibali vya ujenzi vipatikane ndani ya mwezi mmoja, tofauti na kutokupatikana ndani ya mwezi mmoja iwe kwa Mwananchi mwenyewe kushindwa kukamilisha nyaraka zake, na ninataka ikifika tarehe 1 Julai tuzindue mpango utakaomfanya Mwananchi kuweza kufanya maombi yake ya kibali cha ujenzi kupitia mtandao, na kisha atajibiwa na kama kuna mahojiano ataitwa na taratibu zitakapokamilika atapatiwa kibali chake haraka.
  3.  Maeneo mliyoyatenga na kuyaacha kwa ajili ya shughuli za Umma, wekeni mkakati madhubuti na mhakikishe hayavamiwi.
  4. Maeneo yote ya wazi ambayo mlishiriki kutoa hati, nataka ripoti siku ya Ijumaa, kila Manispaa iseme ina viwanja vingapi na vipo wapi.
  5. Waziri wa TAMISEMI aliagiza kupimwa kwa maeneo yote ya Umma, lakini siioni kasi ya upimaji kwenye maeneo hayo, sasa naagiza Wakuu wa Idara kuhakikisha maeneo yote ya Umma yanapimwa kwa haraka.
  6. Nawaagiza Wakuu wa Idara kuongeza bidii kuwatambua wapimaji binafsi wenye sifa na vigezo vya upimaji na pia kuwaelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa upimaji maeneo yao ili waweze kuwa na uhakika wa umiliki wa maeneo yao.
  7. Mambo matatu yamebadilika kwenye Mawizara,moja ya mambo hayo ni mabadiliko ya kisera na sheria, hivyo tuyaangalie kwenye utoaji wa huduma
  8. Mwanasheria uangalie namna tunavyoweza kufanya mabadiliko kwenye Mabaraza yetu ya Kata ili tuendane na kasi ya utoaji huduma.
  9. Natamani kila Mtumishi afanye kazi yake kiuaminifu,kujiamini na atambue dhamana aliyopewa ni kubwa sana.
  10. Kila Mkuu wa Idara aipitie Ilani ya Chama cha Mapinduzi ajue nini kinaihusu Idara yake, na pia ahakikishe Watumishi waliopo kwenye Idara yake wanaijua vizuri Ilani ya Chama na ibara zinazowahusu
  11. Ningependa kufahamu utaratibu wenu wa upandaji wa madaraja na stahiki zenu wakati wa likizo.
  12. Watumishi wote lazima muheshimu Mamlaka mlizonazo, muheshimu Kiongozi wako na tumia vikao halali kutoa taarifa.
  13. Muwe na ushirikiano na Idara nyengine mnazohusiana nazo ilimtengeneze utaratibu wa pamoja wa kutoa huduma kwa Wananchi.
  14. Kwenye utoaji wa hati na taratibu zilizotumika,kama kuna Mtumishi alihusika na utoaji wa hati kinyume na utaratibu, ana wiki moja ajitokeze na aje aniambie changamoto zilivyokuwa
  15. Hakikisha mnawaelimisha na kuwashirikisha Madiwani kama kuna jambo ili mtende haki bila upendeleo.
  16. Wakuu wa Idara, kila mwisho wa wiki Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya wapate taarifa juu ya idadi ya migogoro iliyoshughulikiwa, aina ya changamoto zilizojitokeza, hatua zilizochukuliwa, Watu walioshughulikia na walioshughulikiwa na namba zao za simu ziwepo.
  17. Mimi binafsi na kwa niaba ya Raisi Magufuli tunategemea sana mtufanye tutembee kifua mbele











Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi