Na: Hashim Jumbe
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
UMITASHUMTA Wilaya ya Ilala, Ndugu Msongela Palela, amewaasa Wanafunzi 120
walioingia kambini kujiandaa na mashindano ya UMITASHUMTA kuzingatia nidhamu na
maelekezo mengine watakayopewa na Wasimamizi wao.
Nasaha hizo za Mkurugenzi amezitoa wakati akiwaaga Wanamichezo
hao kabla ya kuingia kambini kujiandaa na mashindano yanayotarajiwa kuanza siku
ya Jumanne ijayo kwa Kanda ya Dar-es-Salaam.
“Nidhamu ndiyo kila kitu kwenu, nataka safari hii kikombe
cha ushindi wa nidhamu kije kwetu Wilaya ya Ilala, mkazingatie maagizo ya
Walimu wenu, mcheze kwa bidii na mtakaporudi nitakuja kuwapokea, na ninawaahidi
kuwapa zawadi ya kwangu Mkurugenzi” alisema Mkurugenzi Palela.
Aidha, Mkurugenzi Palela aliendelea kuwasisitiza Wanafunzi
hao pamoja na kujituma kwenye michezo wakumbuke pia kufanya jitihada kwenye
taaluma “Mimi leo ni Mkurugenzi wenu, najisikia faraja sana Ofisini kwangu
wanapokuja Walimu walionifundisha na kuwasaidia, natamani na nyie siku moja
muwe Wakurugenzi na mje mnisaidie, muwasaidie na Walimu wenu”
Wakati huo huo, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala,
Bi.Elizabeth Thomas ametoa motisha kwa Wachezaji hao kwa kununua kila goli
litakalofungwa kama alivyofanya mwaka jana “mwaka jana mlishinda makombe saba, nataka
na mwaka huu mkashinde makombe yote, na ninatoa ahadi ya kununua kila goli,
mwaka jana kikombe cha nidhamu kilienda Kinondoni, sasa nataka mwaka huu kije
Ilala”.
Ikumbukwe, mashindano ya umoja wa michezo na taaluma kwa
shule za msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yalianza kwa ngazi Kata, Klasta, Wilaya
na sasa ni ngazi ya Mkoa na ngazi ya Kitaifa mashindano yanatarajiwa kufanyika
Jijini Mwanza katikati ya mwezi Juni.