ALIYOYAZUNGUMZA WAZIRI KAIRUKI SIKU YA KWANZA YA ZIARA YAKE MANISPAA YA ILALA

Na: Hashim Jumbe
Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala bora, Mhe. Angellah Kairuki leo ameianza ziara ya siku tatu ndani ya Manispaa ya Ilala kwa lengo la kukutana  na Watumishi na kuzungumza nao. Siku ya kwanza ya ziara hiyo, Mhe. Kairuki amekutana na Watumishi waliopo Jimbo la Ilala na kuongea nao mambo mbalimbali.
Taarifa ifuatayo ni kwa kifupi aliyoyazungumza Mhe. Angellah Kairuki;

1. Tuliona twende hivi kwa kutambua uwingi wa Watumishi waliopo DSM , wenyewe mmeeleza Ilala mpo takribani Watumishi zaidi ya 8,000, kwa hiyo mtakuja kuangalia hapa mpo takribani 10% au 15% kwa hiyo bado, lakini kwa kuwa ndiyo kwanza tunaendelea , ni imani yangu tunaweza kuwafika wote, tunawashukuru.

2. Ndugu zangu, nafasi hii ni adhimu sana kwenu, niwaombe muweze kuitumia vizuri kuweza kuwasilisha, endapo mna kero mbalimbali ili tuweze kuzishughulikia na kuwahudumia.

3. Wapo watakaopata fursa ya kuzungumza na nitaomba kwa kweli wawe huru sana wazungumze.

4. Tunamshukuru Mkuu wa Wilaya na Uongozi wake kwa kikao katika wiki ya Utumishi wa Umma, nimeelezwa hapa mmewasikiliza Watumishi zaidi ya 450, lakini mmeweza kuwasikiliza  Wananchi zaidi ya 249, tunawashukuru sana na jambo la kuigwa na kuchukuliwa mfano na Wilaya nyengine.

5. Niwapongeze zaidi kwa kutenga siku ya Alhamisi ya kila juma kuweza kusikiliza kero mbalimbali. Tunapofanya hivi kwa kiasi kikubwa kero zitakuwa ni chache, lakini tuna uhakika hapatakuwa na kero ambayo itakaa muda mrefu bila kushughulikiwa.

6. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza tija katika Serikali pamoja na ufanisi.

7. Kama Ofisi ya Rais Utumishi, tunaendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa wetu mbalimbali wa Utumishi waliopo Serikalini, tumekuwa tukiwafundisha katika masuala mengi yanayohusu usimamizi wa rasilimali Watu pamoja na maendeleo ya Utumishi

8. Lakini pamoja na mambo mengine, tumewafundisha pia namna bora ya kufanya uhakiki kwa Watumishi wa Umma na kwa sasa wanachokifanya ni kuoanisha taarifa za utambulisho wa Taifa (NIDA) pamoja na mfumo wetu wa masuala ya kiutumishi na mishahara 'lawson'

9. Niwapongeze Jiji, mmefikia takribani 9% na zaidi kwa Watumishi 212 kati ya 226 wameshaoanisha taarifa, lakini kwa upande wa Manispaa bado hawajafika 50% mna takribani 40%, niwaombe sana tujitahidi.

10. Zoezi hili la kuoanisha taarifa ni la muhimu kwenu pia, lakini pamoja na umuhimu kwetu kama Serikali kuhakikisha tuna taarifa sahihi, lakini niwaombe na nyinyi kutoa ushirikiano ili muweze kujiridhisha tarehe zenu za kuzaliwa, kuajiriwa, kupanda daraja

11.Tunayo mifumo yetu ya usajili kupitia RITA, Uhamiaji, Baraza la Mitihani, tungependa mifumo hii sasa izungumze

12. Nipende kusema uhakiki tumeshamaliza na ndiyo maana tunaendelea na hatua nyengine za maendeleo katika utumishi.

13. Tumeeleza vizuri kuhusu mfumo wetu mpya wa ulipaji wa mishahara 'Government Salary Payment Platform' kupitia mfumo huu sasa hivi mishahara ya Watumishi itaingia moja kwa moja kwenye akaunt kutokea benki kuu kinyume na zamani zilipokuwa zinapitia kwenye benki za biashara

14. Faida ya mfumo huu mpya wa malipo ya mishahara, hakutokuwa na utofauti wa ulipwaji wa mishahara kati ya Mtumishi mmoja na mwengine, isitokee mmoja akalipwa leo na mwengine baada ya siku saba.

15. Lengo letu lengine ni kuondokana na madeni na malimbikizo ya mishahara.

16. Katika mfumo wetu wa 'lawson' tunaendelea kusanifu na kuufanyia maboresho.

17. Niwashukuru kwa namna mlivyoendesha  zoezi la uhakiki kwa wenye vyeti kuanzia kidato cha nne, sita na ualimu.

18. Nipende tu kueleza mmeeleza maombi yenu ya ikama. Tumeshatoa kibali kuziba pengo, kwa upande wa Manispaa ya Ilala tunawapatia nafasi 98, lakini hii imeangalia ikama yenu ilivyo.

19. Kwa upande wa ajira mpya kwa mwaka wa fedha 2018/19 tutawapatia kibali cha kuajiri Watumishi 218.

 20. Kwa upande wa 'promotions' natambua kuwa ni kiu kubwa ya wengi, mmeeleza hapa mnatarajia nafasi 1847, mtapata ondoeni shaka.

21. Tumezindua tovuti kuu ya Watumishi ambayo ni kama dirisha ndani ya tovuti kuu ya Wizara ya Utumishi, na lengo lake kuu ni kutoa taarifa za Kiutumishi, lakini pia kila Mtumishi aweze kuwa na uwezo angalau wa kuangalia taarifa zake kwenye mfumo wa 'lawson'

22. Lengo jengine la tovuti ni kuwa na uwazi, lakini pia Mtumishi anaweza kuwasilisha malalamiko yake

23. Nasisitiza mafunzo kwa Watumishi bado yapo, ila ombi langu mpango wa mafunzo uwe wazi kwa Watumishi.












1 Maoni

  1. Suala la mh waziri kutembelea watumishi latia moyo lakn bado utekelezwaj wa changamoto za watumishi maaana jali sio nzr kwa watumish

    JibuFuta
Mpya zaidi Nzee zaidi