Mhe. Dkt. Biteko azindua Zahanati ya Bungoni

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ameishukuru Taasisi ya African Relief Tanzania kwa kushirikiana na Rahma International Society ya nchini Kuwait pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kufanikisha ujenzi wa Zahanati ya Bungoni ambayo itawanufaisha wananchi zaidi ya 12,000 wa kata ya Ilala na maeneo jirani.


Mhe. Biteko ameyasema hayo leo tarehe 29 Desemba, 2023 alipokuwa akizindua Zahanati hiyo iliyopo Kata ya Ilala na kuongeza kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa umbali mfupi zaidi.


Akiongea na wananchi katika uzinduzi huo Mhe. Biteko amesema "Serikali imewasogezea huduma ya afya karibu hivyo niwatake wananchi kutumia fursa ya uwepo wa zahanati hii badala ya kwenda mbali kufuata huduma za afya, kwani ni dhamira ya Serikali kusogeza huduma kwa wananchi.


Vilevile niwaombe viongozi wenzangu tuliopewa dhamana na Rais kuhakikisha tunawahudumia kwa vitendo wananchi na kuinua hali za wanyonge kwa kuwapatia huduma bora wanazostahili.” Ameeleza Mhe. Biteko.

Sambamba na hilo amesema “Niwashukuru Taasisi ya Africa Relief Agency, Rahma International kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ilala, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi kwa kujenga zahanati hii itakayohudumia waananchi zaidi ya 12,000 na Zahanati hii itatoa huduma za maabara, Huduma za Mama na Mtoto pamoja kupima Virusi vya UKIMWI."


Awali akifungua uzinguzi huo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika Wilaya ya Ilala.


Awali, akitoa taarifa ya mafanikio ya Idara ya Afya kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji Dkt. Zaituni Hamza amesema kuwa wamefanikiwa kujenga jumla ya vituo vipya saba vya kutolea huduma na kupandisha hadhi zahanati tano kuwa vituo vya afya, hivyo kufanya jumla ya vituo vya afya kuwa 12.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi