WAMACHINGA WILAYA YA ILALA WAPONGEZA UTENDAJI KAZI WA MHE. RAIS MAGUFULI

Na: Hashim Jumbe
Wafanya biashara ndogo ndogo kwenye soko la Kariakoo maarufu kama Wamachinga, wameitumia siku ya leo kufikisha salamu zao za pongezi kwa Muheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Magufuli kutokana na utendaji kazi wake na usimamiaji wa rasilimali za nchi.

Pongezi hizo zimetolewa mbele ya Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki aliyekuwa Mgeni Rasmi wakati Wamachinga hao wakitoa salamu zao za pongezi kwenye hafla iliyofanyika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo Mnazi Mmoja.

Ifuatayo ni Hotuba fupi iliyotolewa na Waziri Kairuki
  1. Ndugu zangu Wamachinga na Bodaboda awali ya yote, kwanza niwapongeze na niwashukuru sana kwa kuweza kuandaa tukio hili kubwa la kihistoria. Mmeweka historia, mmeweka alama kuonesha ni namna gani mnamuunga mkono, Rais wetu mpendwa Mhe. Magufuli. 
  2. Salamu hizi amezipata, angependa sana kujumuika nanyi kupokea salamu hizi mwenyewe, lakini bahati mbaya amepatwa na majukumu mengine, lakini Inshaallah siku moja tutaweza kuwa naye.
  3. Kwanza kabisa niwapongeze kwa kupongeza jitihada hizi na hatua thabiti, si jambo jepesi na mliweza kumsikia mwenyewe juzi alipoeleza wakati anatoa vyeti kwa Wajumbe wa Kamati walioshiriki katika Tume mbalimbali za Madini pamoja na Kamati ya Majadiliano ya Barick, ye mwenyewe mmemsikia akisema alitikisika.
  4. Si jambo jepesi na Mtu akifanya jambo kubwa na zito, uungwana ni kumpongeza, uungwana ni kumtia moyo ili aweze kwenda mbele zaidi na kutuletea mambo makubwa zaidi.
  5. Nikupongeze Mkuu wa Wilaya pamoja na Uongozi mzima wa Mkoa kwa kuweza kuridhia Wamachinga hawa na bodaboda waweze kufanya tukio kubwa na la kihistoria, naamini msingewaunga mkono isingeweza kuwa jambo jepesi.
  6. Nichukue fursa hii kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Ilala, nakupongeza sana, kwanza kabisa kwa namna unavyowaongoza wapiga kura wako, kwa kuangalia tu hapa unaona kabisa Ilala ni shwari.
  7. Lakini pili, nimeyasema haya, mnaye Mbunge makini, mnaye Mbunge mwenye uwezo, katika sakata hili la swala zima la Madini na utoroshaji Madini, Mhe. Zungu aliongoza Tume ya Mhe. Spika iliyokuwa ikichunguza suala zima la biashara ya Almasi na mlishuhudia, mliona matokeo ya Tume ile na mliona matokeo ya ripoti ya Tume aliyoiongoza.
  8. Mimi nipende tu kusema kama Serikali na kupitia Wizara ya Madini, tunakushukuru wewe, tunakushukuru pia Mhe. Spika kwa namna ambavyo mmeweza pia kutuwekea njia na misimamo mbalimbali kwa Sekta ya Madini ya Almasi.
  9. Lakini pili, kuwa mkishuhudia Mhe. Rais ameunda Kamati mbili, Kamati moja ya Prof. Mruma na nyengine ya Prof. Ossoro na ukiangalia Kamati hizi zimeweza kufanya kazi kubwa kuweza kutupatia masuala mazima kuhusiana na Makinikia ya Dhahabu na Shaba.
  10. Michanga iliyokuwa inasafirishwa nje ya Nchi, lakini tulikuwa hatufahamu endapo mchanga huo unapoondoka kuna Madini kiasi gani katika mchanga huo? na hivi pia kwa uamuzi wa Mhe. Rais alipoweka zuio la kusafirisha mchanga huo, tumeweza kushuhudia mafanikio mpaka hapa tulipofika na leo hii tunampongeza kwa kuweza kupata mafanikio ya kupata Bilioni 700
  11. Lakini pia tumeona Mhe. Rais alipounda Kamati ya Majadiliano baina ya Serikali na Barick, Kamati ambayo iliongozwa na Prof. Kabudi, Waziri wetu wa Katiba na Sheria pamoja na Wajumbe wengine ambao mmeona Mhe. Rais amewapatia vyeti kwa ajili ya kutambua mchango wao muhimu walioufanya katika majadiliano hayo, ukiangalia kwa hakika na wenyewe hawakulala usiku na mchana kuweza kutupa kile ambacho Watanzania tunakistahili
  12. Bilioni 700 si ndogo, tukisema tumezipeleka kwenye barabara tu, ni ujenzi wa barabara takribani Kilomita 700 hivi, ukikaa peke yako hivi inawezekana tu ungezipata? lakini kwa uamuzi wa Mhe. Rais tumeweza kuona tutaweza kulipwa takribani Bilioni 700 ambazo zinaweza kutusaidia katika huduma mbalimbali za Kijamii.
  13. Lakini pili, kwanza ni kukubali wenyewe kuweza kutekeleza Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017 ambapo kupitia marekebisho hayo ya Sheria ya Madini, tumeweza kuona Serikali itaweza kupata hisa za 16% katika Migodi ya Barick ambayo ni Bulyanhulu, North  Mara pamoja na Buzwagi
  14. Lakini tatu, huko nyuma walikuwa wakiweka fedha zao nje ya Nchi, sasa fedha zao zote za kigeni zitawekwa hapa hapa Nchi kupitia Benki Kuu na tunaamini hii itaweza kuongeza mzunguko wa fedha za kigeni kwenye Benki zetu, vile vile iweze kutusaidia na Sisi kuweza kupata mikopo na masuala mengine ya Kiuchumi.
  15. Lakini vile vile Barick na Serikali, faida yote itakayopatikana katika Migodi yote ya Barick tutaweza kugawana faida kati ya Serikali na Barick kwa Asilimia 50 kwa 50 baada ya kuondoa malipo ya kodi na tozo ambazo Barick wanastahili kuzilipa kwa mujibu wa Sheria.
  16. Lakini pia, Wataalamu wetu wa Serikalini wataweza kushiriki kusimamia Migodi ya dhahabu inayomilikiwa na Barick katika ngazi za juu za Uongozi, badala tu ya kukaa na kutoshiriki katika Menejimenti za Migodi hiyo, hilo tunaamini litatusaidia kujua yanayoendelea katika Migodi hiyo, lakini pia itatusaidia kuendelea kuwajengea uwezo Wataalamu wetu Wazalendo, Wazawa kuongoza  Migodi hiyo.
  17. Lakini vile vile tutaweza kupata ajira nyingi kwa Watanzania katika Migodi ya Barick iliyopo hapa Nchini.












Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi