MANISPAA YA ILALA YAPIGA MARUFUKU UFANYAJI WA BIASHARA NDOGO NDOGO MAENEO YOTE YA KATIKATI YA MJI ‘CBD’

Na: Hashim Jumbe

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, wametoa tamko la kuwapiga marufuku Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama ‘Wamachinga’ kuendelea na biashara katika maeneo yote ya katikati ya Mji  ‘CBD’, maeneo hayo ni pamoja na Kariakoo, Mchikichini, Gerezani, Mchafukoge, Kisutu, Kivukoni, Ilala, Buguruni, Upanga Mashariki na Upanga Magharibi.

Tamko la kuwapiga marufuku Wafanyabiashara hao limetolewa leo na Uongozi wa Manispaa ya Ilala baada ya kufanyika makubaliano ya pamoja kati ya Viongozi wa Manispaa ya Ilala  na Viongozi wa Wafanyabiashara hao.

Akiongea wakati wa Mkutano na Waandishi wa habari, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Mhe. Charles Kuyeko alieleza kuwa Manispaa ya Ilala sasa imefanya maandalizi yanayoridhisha kwaajili ya kuwaondoa Wamachinga katika maeneo yote ya katikati ya mji na kuelekeza maeneo yaliyotengwa kufanyia biashara hizo ndogo ndogo. Maeneo hayo ni Soko la Kigogo freshi, Kivule, Tabata Muslim na Ukonga Magereza.

Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Bw. Isaya Mngurumi alisema Manispaa ya Ilala imeshapeleka miundombinu ya maji, vyoo na barabara katika maeneo yaliyoelekezwa kufanywa biashara, huku akisisitiza Wafanyabiashara waanze kuondoka kuanzia kesho na itakapofika siku ya jumamosi Manispaa haitosita kutumia nguvu kuwaondoa Wafanyabiashara hao, ikiwa ni kuwakatama na kuwafungulia mashtaka.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Mhe. Charles Kuyeko akitoa ufafanuzi kuhusiana na namna Manispaa ya Ilala itakavyowaondosha Wamachinga maeneo ya katikati ya Mji





Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi