MANISPAA YA ILALA YAWAAPISHA WENYEVITI NA WAJUMBE WA KAMATI ZA MITAA, MKURUGENZI AWAASA KUSIMAMIA HAKI

Na: Hashim Jumbe
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, leo imewaapisha Viongozi wake wa Mitaa ambao ni Wanyeviti wapya 12 wa Kamati za Mitaa pamoja na Wajumbe 35 wa Kamati za Mitaa.Viongozi hao wapya wametokana na kuchaguliwa kwenye Uchaguzi mdogo uliofanyika tarehe 16 Novemba, 2017 ikiwa ni kuziba nafasi zilizoachwa wazi kwenye Mitaa hiyo 12 kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufariki kwa Wenyeviti waliokuwepo awali na wengine walioondoka kwenye nafasi zao na kwenda kutumikia nafasi nyengine.

Kiapo hicho cha Utii na Uadilifu kwa Viongozi hao wa Mitaa, ni maelekezo ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati za Mtaa katika Mamlaka za Miji za mwaka 2014 Ibara ya 30, kifungu cha 2.

Aidha, ikumbukwe Mitaa iliyokuwa ikifanya Uchaguzi huo ni Mitaa 12 kutoka kwenye Kata 7 za Manispaa ya Ilala, na Mitaa hiyo ni;- Bonyokwa, Twiga, Relini, Kasulu, Mongolandege, Amani, Kitinye, Machimbo, Kipunguni B, Kivule, Kerezange na Bombambili.

Akiongea wakati wa zoezi hilo la kula kiapo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Ndugu Msongela Palela aliwaasa Viongozi hao wa Mitaa kwenda kutenda haki kwa Wananchi waliowachagua "nyinyi ni Viongozi wa kuchaguliwa  na Wananchi, wamewachagua nyinyi kwa kuwa wana imani kubwa kwenu. Wanaamini kuwa mtakuwa Viongozi katika kutatua changamoto zinazowakabili, lakini pia mtakuwa Viongozi katika kutoa na kuibua Mipango ya Maendeleo katika maeneo yenu ya Utawala"

Mwisho, Mkurugenzi Palela alitoa rai kwa Viongozi hao "natoa rai kwenu, kuwa mnapaswa kutekeleza wajibu na majukumu mliyokasimiwa na Wakazi katika Mitaa yenu kwa Utii na Uadilifu mkubwa"
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Ndugu Msongela Palela akiongea na Wenyeviti pamoja na Wajumbe wa Kamati za Mitaa kabla ya kuanza zoezi la kuwaapisha
Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Wakili Bonaventure Mwambaja akitoa muongozo wa kiapo cha Utii na Uadilifu namna kinavyokuwa na masharti yake
Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Wakili Mwambaja akiongoza Kiapo cha Utii na Uadilifu kwa Wenyeviti wapya wa Kamati za Mitaa







Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Edward Mpogolo akitoa nasaha zake kwa Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Mitaa mara baada ya kula kiapo

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi