Na: Hashim
Jumbe
KWA mujibu wa Sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2012, Dar es
Salaam inakadiriwa kuwa na Watu wapatao Milioni 4.3, huku idadi hiyo
ikitazamiwa kuongezeka hadi kufikia Watu Milioni 10 ifikapo mwaka 2030, hivyo
kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kati ya Majiji yanayoongoza kwa ukubwa na
makazi mengi.
Sambamba na ongezeko hilo, lakini pia Jiji la Dar es Salaam
ndiyo Jiji linalochangia kwa asilimia kubwa katika ukuaji wa pato la Taifa na
kuwa lango la biashara kwa Mataifa ya jirani, huku Jiji hilo likikabiliwa na
changamaoto ya ubora wa Miundombinu, hivyo kuzorotesha baadhi ya shughuli na
kuwa kikwazo kwa ustawi wa Jiji na Taifa kwa ujumla.
Aidha, kasi ya ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam haiendani na
Miundombinu iliyopo kwani inakadiriwa kuwa asilimia kati ya 70 hadi 80 ya
makazi ya Jiji la Dar es Salaam hayajapimwa, hivyo kutokana na ukuaji huo na
mabadiliko ya tabia nchi yanayoikabili Dunia, athari za mafuriko zinatarajiwa
kuongezeka katika Jiji la Dar es
Salaam, kwa hali hiyo bila ya kuwa na mipango bora ya utoaji wa huduma, Jiji
hili linaweza kutokukalika.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania ndipo ilipokuja na wazo la kuwa na Mradi wa Uendelezaji wa
Jiji la Dar es Salaam ujulikanao kama ‘Dar es Salaam Metropolitan Development
Project’ ama unaweza kuuita kwa kifupi DMDP.
Aidha, Mradi wa DMDP ni
matokeo ya miradi miwili mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Tanzania. Mradi
wa kwanza ni ule wa uendelezaji wa Miji minane kimkakati (Tanzania Strategic
Cities Project – TSCP) unaotekelezwa katika Majiji ya Arusha, Mwanza , Tanga na Mbeya
na Manispaa za Kigoma Ujiji, Mtwara Mikindani, Dodoma pamoja na
Mamlaka ya Uendelezaji wa Makao Makuu Dodoma – CDA.
Mradi mwingine ni ule wa
Uendelezaji Miji kumi na nane ujulikanao kama Urban Local Government
Strengthening Programme (ULGSP). Kwa ujumla miradi hii yote mitatu ina lengo la
kuboresha miundombinu ya barabara, mitaro ya maji ya mvua, nyenzo muhimu za
ukusanyaji na uhifadhi wa taka ngumu pamoja na mifumo ya ukusanyaji wa mapato
ya ndani katika maeneo husika vimeboreshwa kwa kiwango kikubwa.
Maandalizi ya mradi wa
DMDP
Maandalizi ya Mradi wa DMDP
ambao umeanza kutekelezwa katika Manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam
yalianza katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2012/2013 kwa Manispaa za Jiji la
Dar es Salaam kuibua vipaumbele kuanzia ngazi ya chini na kufuatiwa pembuzi na sanifu
zilizofanywa na Washauri waelekezi mbalimbali.
Vigezo muhimu vilivyozingatiwa vilikuwa ni hivi
vifuatavyo:-
i) Miradi inayounganisha maeneo ya Watu wenye kipato
kidogo na yaliyojengwa holela
ii) Miradi inayounganisha Wilaya na Mkoa
iii) Miradi inayounganisha maeneo mbalimbali na ukanda wa mabasi
yaendayo haraka (BRT) ili kurahisisha usafirishaji
Kwa Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala, vigezo hivyo vitatu viliibua miradi ifuatayo;
i) Ujenzi wa barabara za mlisho (feeder roads) zenye urefu
wa kilometa 3.2
ii) Ujenzi wa mifereji ya kutiririsha maji ya mvua yenye urefu
wa kilometa 15.96 katika mabonde ya mto Msimbazi na Yombo
iii) Kupandisha hadhi makazi yaliyopangwa kiholela katika Kata
za Gongolamboto, Kiwalani, na Ukonga, kuweka nyenzo za ukusanyaji wa taka
ngumu, kujenga mitaro ya kutiririsha maji ya mvua, kuweka taa za barabarani,
kujenga njia za watembea kwa miguu, ujenzi wa maeneo ya mapumziko na vituo vya
mabasi, ujenzi wa vyoo vya umma na ujenzi wa maeneo ya michezo.
iv) Kuandaa Mpango kabambe wa Mfumo wa Maji ya Mvua na Maji Taka
(Storm Drainage and Sewerage Master plan)
v) Kundaa Mpango Mkakati wa kuendeleza Ukanda wa mabasi yaendayo
haraka (BRT Corridor Development Strategy). Kwa kushirikisha Sekta Binafsi;
kujenga masoko ya kisasa na ya kawaida, kujenga maduka makubwa (shopping
malls) na ya kawaida, kuboresha maeneo ya utalii, kujenga maeneo maalum ya
maegesho, kuweka njia za waendesha baiskeli na watembea kwa miguu n.k
vi) Kufunga mfumo wa kisasa wa ukusanyaji wa mapato wa
Halmashauri
vii) Kujenga uwezo wa mwitikio wa haraka katika kukabiliana na
majanga.
Utekelezaji wa Mradi
wa DMDP kwa Manispaa ya Ilala
Kwa ujumla utekelezaji wa Mradi wa DMDP umepangwa kufanyika
katika awamu mbili. Awamu ya kwanza imeanza kutekelezwa katika kipindi cha
miaka mitano kuanzia 2016 mpaka 2020 na awamu ya pili inatarajiwa kutekelezwa
kuanzia mwaka 2020 mpaka 2025 kadri ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania
na Benki ya Dunia.
Manispaa ya Ilala imetengewa Shilingi Bilioni 115 kwa mradi wote na hadi sasa imeingia mikataba yenye
thamani ya Shilingi Bilioni 49.84
katika kujenga Kilometa 25.84 za barabara za lami, kujenga masoko 3, kujenga
maeneo ya mapumziko, kujenga mifereji ya chini ya Kilometa 2.8 (underground
storm drainage), kuweka huduma za vyoo vya Umma na maji safi.
Aidha, Shilingi Bilioni
65.16 zimepangwa kujenga barabara ya Ulongoni Bangulo-Kinyerezi yenye urefu
wa Kilometa 7.5 na kujenga mifereji mikubwa ya maji yenye urefu wa Kilometa
15.96 pamoja na bwawa la kukinga maji kwa muda (Detention pond)
Hadi kufikia Machi, 2018 kwa Manispaa ya Ilala mradi wa DMDP
umetekelezwa kama ifuatavyo;
i. Ujenzi wa barabara za Mlisho (feeder roads) zenye urefu wa
Kilometa 3.2 ambazo ni Ndanda yenye urefu wa Kilometa 0.35, Kiungani Kilometa
0.68, Omari Londo Kilometa 0.53, Olympio Kilometa 0.68, Mbarouk Kilometa 0.38
na barabara za Kongo, Livingstone, Swahili na Nyamwezi zenye jumla ya urefu wa
Kilometa 0.58. Pamoja na barabara hizo, lakini pia ujenzi wa mifereji ya chini
(underground storm drainage) yenye urefu wa Kilometa 0.58 imekamilika sambamba
na ujenzi wa Ofisi na maabara ya kisasa. Gharama zilizotumika hadi sasa ni
Shilingi Bilioni 7.18
Moja kati ya barabara za mlisho iliyojengwa Kata ya Upanga Mashariki, barabara ya Olympio inavyoonekana kwa sasa baada ya kujengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam 'DMDP' |
ii. Ujenzi wa barabara kwenye makazi yasiyopangwa
Kata ya Gongolamboto ambapo ujenzi huo ulianza tangu tarehe 1 Novemba, 2017
ambapo ujenzi umeanza kwenye barabara za Chung'e iliyo na urefu wa Kilometa
1.49, barabara ya Kampala Kilometa 2.06, Limbanga 2.44, High Mount Kilometa
1.44 na Baghdad Kilometa 0.34. Aidha Kata ya Gongolamboto pia unajengwa mtaro
wenye urefu wa Kilometa 1.85, vizimba 7 vya taka na kununua garimoja la kusomba
taka. Gharama zilizotumika hadi sasa ni Bilioni
3.05
|
Barabara ya Kampala yenye urefu wa Kilometa 2.06 nimoja kati ya barabara zilizojengwa kwenye maeneo yasiyopangawa kwenye Kata ya Gongolamboto |
iii. Ujenzi mwengine ni kwenye barabara zilizopo
kwenye makazi yasiyopangwa Kata ya Kiwalani ambapo barabara zenye urefu wa
Kilometa 10.35 zinaendelea kujengwa, barabara hizo ni zile za Bush iliyo na
urefu wa Kilometa 1.07, Gude Kilometa 1.33, Jongo Kilometa 0.4, Mbilinyi
Kilometa 0.35, Pepsi Kilometa 0.59, Jamaka Kilometa 0.62, Zahanati Kilometa
1.17, Kamungu Kilometa 1.21, Mkwajuni Kilometa 1.16, Binti Musa Kilometa 2.14
na Betheli Kilometa 0.31
Barabara ya Gude yenye urefu wa Kilometa 1.33 ni moja ya kati ya barabara zilizojengwa kwenye Kata ya Kiwalani |
iv. Aidha, Kata ya Kiwalani pia itanufaika na
ujenzi wa vituo vitatu vya kutolea huduma za vyoo, vizimba 8, kununua gari 1 la
kusombea taka,kujenga masoko matatu, kujenga maeneo ya kupumzikia mawili na
kujenga vituo vitatu vyaa kutoleaa huduma za maji safi. Hivyo jumla ya fedha
zilizotumia kwa Kata hii ya Kiwalani hadi sasa Shilingi Bilioni 2.8
v. Kata nyengine inayonufaika na Mradi huu wa DMDP
ni Ukonga ambapo hadi sasa maeneo yaliyotekelezwa ni ujenzi wa barabara ya
Kilometa 12.29 kwenye makazi yasiyopangwa ambapo zinajengwa barabara za Markaz
yenye urefu wa Kilometa 1.86, Zimbili yenye urefu wa Kilomita 3.02, Dispensary
yenye urefu wa Kilometa 1.06, School yenye urefu wa Kilometa 2.18 na Chacha
Kilometa 3.17
Ujenzi wa baraba ya Zimbili iliyo na urefu wa Kilometa 3.02 ukiendelea |
vi. Ujenzi mwengine kwa Kata ya Ukonga ni wa vituo
7 kwa ajili ya Wananchi kupata huduma safi za maji na ujenzi wa vizimba 9 vya
taka, hivyo kufanya jumla ya gharama iliyotumia kwa Kata hiyo hadi sasa kufikia
Shilingi Bilioni 2.95