IDARA YA ELIMU MSINGI MANISPAA YA ILALA YAWAPATIWA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO WALIMU 65 WALIOKUWA WAKIFUNDISHA SHULE ZA SEKONDARI

Na: Hashim Jumbe
Idara ya Elimu Msingi Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi ADEM kilichopo Bagamoyo, leo wamekamilisha mafunzo ya siku tano (5) yaliyolenga kuwajengea uwezo Walimu Sitini na Tano (65) waliohama kutoka Shule za Sekondari na kuhamia Shule za Msingi, kufuatia agizo la Serikali la kuwahamisha Walimu wa ziada katika masomo ya sanaa kwenye Shule za Sekondari, hivyo Walimu hao wamekwenda Shule za Msingi kupunguza upungufu uliokuwepo.

Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala, Bibi. Elizabeth Thomas alisema "Baada ya Walimu hawa kupokea barua, wameripoti vituoni na wapo tayari kufundisha Shule za Msingi. Kwa kuwa Walimu wametoka kufundisha Wanafunzi wakubwa wa Sekondari, basi Idara ya Elimu Msingi ikaona ni vyema yafanyike mafunzo kwa Walimu hawa ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao wakiwa katika Shule za Msingi"

Aidha, Afisa Elimu huyo aliweka wazi suala na stahiki za Walimu hao ikiwa ni pamoja na pesa ya usumbufu wa kuhama kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine, Bibi Elizabeth Thomas alisema "Walimu hawa wameshatengewa malipo yao na baadhi wameshapokea kupitia benki zao"

Naye Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Hamis Lissu ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi wakati wa kufunga mafunzo hayo alimuagiza Afisa Elimu wa Manispaa ya Ilala kuwaangalia kwa makini Walimu hao na alisisitiza kutokuwabagua Walimu hao "naagiza Afisa Elimu uniletee majina ya Walimu hawa, tuwaangalie kila panapotokea kazi maalum tuweze kuwatumia, maana Walimu hawa wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwetu kwa kukubali agizo halali la Serikali"

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Bw. Msongela Palela aliwaasa Walimu hao kufanya kazi kwa juhudi na wasihuzunike kwa kuhamishwa vituo vyao vya awali vya kazi "Hata Mimi Mkurugenzi wenu nilipopata uhamisho wa kuwa Mkurugenzi niliingiwa na hofu, lakini nikakubaliana nao nikaendelea kujiamini na kufanya kazi kwa weledi"

Mkurugenzi Palela aliendelea kusema "kumekuwa na maneno ya chinichini kuwa mkihamia huku Shule za Msingi ni kama mmekubali kushushwa kiutumishi, naomba niwahakikishie kuwa stahiki zenu zote za kiutumishi zipo palepale na maneno kuwa mmeshushwa hayo yapuuzeni"

Kwa kutambua umuhimu wa mafunzo haya Walimu wameweza kujifunza; Ushauri na unasihi, uchambuzi wa mtaala, uchambuzi wa mihtasari na shughuli za kutendwa na Mwalimu,miongozo ya kufundishia, upimaji wa maendeleo ya Wanafunzi, utunzaji wa kumbukumbu za maendeleo ya Wanafunzi.





















Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi