Kamati ya kudhibiti UKIMWI Manispaa ya Ilala yafanya ziara ya mafunzo Mkoani Lindi

Na: Hashim Jumbe

Ugonjwa wa UKIMWI bado ni tatizo kubwa katika nchi yetu na Duniani kwa ujumla, kwani hadi sasa hakuna tiba wala kinga iliyothibitishwa juu ya ugonjwa huo, huku watu milioni 43.9 wakikadiriwa kuishi na virusi vya Ukimwi Duniani kote, ambapo kwa Tanzania bara hali ya maambukizi ikiwa ni 4.9% na Mkoa wa Lindi ukiwa nafasi ya mwisho kwa kuwa na kiwango kidogo cha 0.3% ya maambukizi.

Katika hali hiyo, ndipo kamati ya kudhibiti UKIMWI Manispaa ya Ilala ilipowalazimu kufanya ziara ya kimafunzo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi na kupata uzoefu wa namna wanavyosimamia masuala yanayohusu UKIMWI kupitia kamati yao ya kudhibiti UKIMWI iliyopo Manispaa ya Lindi.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mji Manispaa ya Lindi Dkt. Zulfa Msami akitoa maelezo mbele ya kamati ya kudhibiti UKIMWI Manispaa ya Ilala namna wanavyotoa huduma za afya na elimu ya kudhibiti maambukizi ya VVU 
Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi imechangia kwa sehemu kubwa kupungua kwa maambukizi kwa ngazi ya Mkoa kutoka 2.9% hadi 0.3% na katika mapambano yake dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI imehakikisha inafuata malengo ya 90, 90, 90 ambapo; 90% ya kwanza ni wenye maambukizi wafahamu hali zao, 90% ya pili ni watakaogundulika na maambukizi ya VVU waanze dawa za ARV na 90% ya mwisho ni ya wanaotumia dawa wawe na idadi ndogo ya VVU chini ya 1000

Pamoja na kupatiwa elimu ya usimamizi wa masuala ya Ukimwi, lakini pia kamati ya kudhibiti UKIMWI Manispaa ya Ilala, walipata pia nafasi ya kutembelea kituo cha afya cha Mji na kituo cha afya cha Mnazi Mmoja na kuhitimisha mafunzo kwa kutembelea machinjio ya kisasa yanayojengwa na Manispaa ya Lindi.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudhibiti UKIMWI Manispaa ya Ilala ambaye pia ni Kaimu Meya wa Manispaa hiyo, Mhe. Omary Kumbilamoto akitoa salamu za Halmashauri mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi walipomtembelea Ofisini kwake
Ikumbukwe kuwa Kamati ya kudhibiti UKIMWI, ndiyo yenye majukumu ya kuhamasisha upimaji wa hiari, kuhudumia Jamii, kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI, kuratibu utendaji kazi wa kamati za kudhibiti Ukimwi katika Kata, kushirikiana na dawati la jinsia katika kupata taarifa mbalimbali za matukio ya udhalilishaji wa jinsia, kutoa lishe kwa Watumishi wanaoishi na VVU waliojitokeza na kushirikiana na mashirika yasiyo na Kiserikali katika mapambano dhidi ya Ukimwi.




Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi