Na: Sabina Misala, Judith Damas
Halmashauri ya Manispaa
ya Ilala imetoa sababu ya kufanikiwa katika ukusanyaji wa mapato kwa mwaka 2018/2019
na ilivyotekeleza miradi ya maendeleo ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu
ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Hayo yamebainishwa na Mchumi
wa Manispaa ya Ilala Bw. Ando Mwakunga wakati akiwasilisha taarifa ya Miradi ya
Kimaendeleo iliyotekelezwa na Manispaa ya Ilala kwa kipindi cha kuanzia Julai
2018 hadi Juni 2019 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne cha
kupitia taarifa za utendaji kazi kilichofanyika leo tarehe 26 Agosti 2019 katika
ukumbi wa Mikutano wa Arnatouglou-Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Aidha, Bw. Mwakunga
alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilipanga kukusanya Shilingi Bilioni
56.2 katika bajeti yake ya mwaka 2018/2019 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
ya maendeleo na kuongeza kuwa Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni
58 ambazo ni sawa na 102% na fedha hizo zimetumika kuongeza chachu katika sekta za
Afya, Elimu Msingi na Sekondari ili
kuleta maendeleo katika kaya za Halmashauri hiyo
“Kama Halmashauri
kipaumbele chetu ilikuwa ni kutekeleza Miradi ya Elimu msingi na sekondari
kutokana na idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza
Manispaa ya Ilala kuwa ni 20,400 na wote walifanikiwa kuingia Sekondari kwa
kuwa tumejenga madarasa na vyoo vya kutosha ili kuhakikisha wanafunzi wanachukuliwa kama walivyochaguliwa” amesema Bw.
Mwankuga.
Pamoja na hayo, lakini
pia Bw. Ando ameeleza kuwa miradi
inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa
ya Ilala ni mingi na kasi ya utekelezaji ni ya kiwango cha juu nakuongeza kuwa
“mimi kama mchumi nasema utekelezaji wa miradi ni mzuri kwani katika miradi ya
Afya tumeweza kujenga vituo vya afya na
zahanati maeneo tofauti kama vile Mbondole, Lubakaya, Kipawa, Mzinga , ambazo
zinasaidia kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wa Manispaa ya Ilala”
Akiendelea kuzungumza,
Mchumi MwankUga amesema kuwa agizo la Serikali
ni kuhakikisha kuwa 10% ya Bajeti ya
Halmashauri inatengwa kwaajili ya Mikopo ya Vijana, Wanawake na wenye ulemavu, kwani katika Bajeti ya
mwaka 2018-2019 10% iliyopelekwa kwa vijana, Wanawake na walemavu ilikuwa ni Shilingi Bilioni 3.7.
“mpaka kumaliza mwaka 2018/2019
mikopo ya vijana, wanawake na walemavu
imepelekwa kwa asilimia 100% na kutolewa kama ilivyoidhinishwa kwenye
Bajeti, hivyo kutekeleza agizo la
waziri wa TAMISEMI la kuhakikisha Halmashauri zote zinapeleka asilimia 100%”
Hatahivyo mchumi
Mwankuga ameongeza kuwa licha ya mafanikio ambayo Manispaa ya Ilala imepata pia
kuna changamoto ambazo zinawakabili na kuhakikisha kuwa wanazitatua, vilevile
mchumi huyo ametoa shukrani zake za dhati kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa
ya Ilala pamoja na Madiwani kwa
ushirikiano wao na kuwaomba waendelee na ushirikiano huo.