Na Lulanga Merecheades, Esha Mnyanga na Ruth Thomas.
Manispaa ya Ilala
jijini Dar es salaam ipo katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Soko la
kisasa la Kisutu. Soko hilo linajengwa
na kampuni ya M/S Mohammed Builders litakalo gharimu jumla ya TSh 13.4 Bilioni
fedha kutoka Serikali kuu.
Soko hilo lipo katika
hatua ya awali ya ujenzi. Akizungumzia ujenzi wa Mradi huo Mchumi wa Manispaa
ya Ilala na Mwenyekiti wa timu ya Usimamizi wa Soko la Kisutu Beatha Ezekia
amesema Soko hilo litachukua muda wa miezi 18 hadi kukamilika kwake, linajengwa katikati ya mji kwani ndiyo kitovu
cha uchumi wa mkoa wa Dar es Salaam na kukamilika kwake kutachukua wafanyabishara
zaidi ya 500, na watakuwa wakifanya biashara zao katika vitengo tofauti tofauti
kulingana na bidhaa zao.
Ujenzi wa soko hilo ni
mpango wa Serikali katika Kuhakikisha kwamba Serikali za Mitaa zinajitegemea
kwa mapato yake ya ndani, hivyo kupitia Mradi huu wa soko la kisasa Kisutu
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala itaweza kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka
Serikali Kuu kwa kuongeza mapato yake ya ndani, kutengeneza fursa za ajira kwa
wananchi Wa Manispaa na Mkoa kiujumla.
Mbali na uwepo wa
shughuli za kiuchumi kama uuzaji wa nafaka, matunda, mbogamboga, kuku hai wa
kisasa na asili, uchinjaji kuku, huduma ya Baba na Mama lishe, kutakuwepo na maduka mbalimbali, Ukumbi mkubwa wa mikutano
pamoja na ofisi mbalimbali. Soko hilo linajengwa kisasa zaidi katika kutimiza
Mahitaji mbalimbali ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla
watakaofika kupata huduma mahali hapo.
Tags:
HABARI