Na: Judith Damas na Rafiki Ally
Idara ya Afya Manispaa
ya Ilala imewasilisha tathmini ya mradi wa TCI kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo
leo tarehe 6 Septemba 2019 katika ukumbi wa Arnatouglou Mnazi Mmoja Jijini Dar
es salaam. Kupitia kikao hicho Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala Dkt Emily
Eliewaha ameelezea lengo la mradi huo wa TCI kuwa ni kuhimiza masuala ya uzazi
wa mpango, lishe bora na huduma rafiki kwa vijana katika Manispaa ya Ilala.
Akifungua kikao hicho
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Bi. Tabu Shaibu amewapongeza
idara ya afya kwa kuanzisha mradi huo ambao unaleta matokeo chanya kwa wananchi
wa Manispaa ya Ilala na hivyo kusisitiza juu ya suala la lishe bora ili kuweza
kuzuia vifo vya mama na mtoto kwa lengo la kuongeza nguvu kazi katika jamii.
Aidha, Bi. Tabu Shaibu
ametoa wito kwa wajumbe wa mradi huo wa TCI hususani wajumbe wa huduma rafiki
kwa vijana waweze kutumia mbinu za kiteknolojia zaidi ili kuboresha huduma hii,
pia amewahimiza wajumbe hao kushirikiana na watu wa TEHAMA ili kukuza mradi huo
na kuhakikisha huduma hii huwafikia vijana wengi wa Manispaa ya Ilala na Nchi kwa ujumla kwa muda muafaka.
Akitoa taarifa za
utekelezaji wa mradi huo, Mratibu Msaidizi wa huduma za afya ya uzazi na mtoto,
Bi. Edith Kijazi amesema kuwa mradi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani
wameweza kutoa elimu ya uzazi wa mpango katika vyombo mbalimbali vya habari
kama TBC1, Sibuka Maisha, City FM na Clouds radio. Pia wajumbe wa mradi huo wa
TCI wamefanikiwa kutoa elimu katika shule mbalimbali na vyuo kwa kuanzisha
vikundi kama vile Chuo cha Kampala, Muhimbili na Kitunda Sekondari kwa lengo la
kuwasaidia vijana wa maeneo hayo kuwa mabalozi wa vijana wengine.
Akitoa ufafanuzi zaidi
juu ya mpango huo unavyo fanya kazi Bi. Rose Mzava amesema kuwa mradi huo
umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani kumekua na ongezeko kubwa la wateja
ukilinganisha na mwaka 2017 ambapo 2017 kulikua na wateja 69185 hivyo
kuongezeka wateja 12013 na hivyo kufikia idadi ya wateja 81198 mnamo mwaka 2018.
Hata hivyo Bi. Mzava ameainisha vituo ambavyo vimeonesha juhudi za utendaji
kazi kuhusu mpango huo kwa kuwa na wateja wengi zaidi kuliko vituo vingine,
vituo hivyo ni Kiwalani, Buyuni na Buguruni. Akiendelea kutoa ufafanuzi huo Bi.
Mzava ametoa ombi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kutenga bajeti ya siku ya
uzazi wa Mpango Manispaa ya Ilala ili kuboresha mpango huo.
Kwa niaba ya Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala, Bi. Tabu Shaibu amekabidhi zawadi kwa wakuu wa vituo
hivyo vilivyo fanya vizuri katika utekelezaji wa mpango huo kwa kuwapa vyeti na
mshindi wa kwanza ambaye ni mwakilishi wa kituo cha kiwalani akipokea zawadi ya
kombe na cheti, pia baadhi ya wajumbe kama vile Janeth Jela, Steven Mapunda na
Flora Amosi wamepewa zawadi ya vyeti kwa kuwa wabunifu na kujituma zaidi katika
kazi kwani wametoa elimu ya uzazi wa mpango katika vituo mbalimbali kama vile
kambi za Jeshi na vituo vya watoto yatima.