Na: Hashim Jumbe
ALIWAHI kusema aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa “Njia nzuri ya kuwapa pesa masikini ni kuwapa watoto wao elimu iliyo bora” hivyo, Rais Dkt. John Magufuli ameamua kuyaishi maneno haya kwa vitendo kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali hadi Kidato cha Nne
Aidha, katika kipindi cha miaka Minne cha Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mambo mbalimbali ya kimaendeleo yameendelea kutekelezwa kama yalivyoainishwa kwenye Mkakati wa Taifa wa kuinua Uchumi, huku Sekta ya Elimu ikiwa ni moja ya Sekta zilizopewa kipaumbele katika ustawi wa Taifa la Tanzania.
Sote tunafahamu, Rais wetu mpendwa Dkt. John
Magufuli amekuwa mkombozi wa kweli kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini ambao walikuwa na wakati mgumu kugharamia masomo ya watoto wao kutokana na hali zao za kimaisha, hivyo elimu bila malipo imekuwa mkombozi wa wengi na teyari imeanza kuleta matokeo chanya yatakayosaidia kuifikia dhamira ya Serikali ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi yatakayoibadilisha nchi yetu na kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Ili kutimiza azma hiyo, Serikali imetoa Miongozo na Nyaraka mbalimbali za Elimu inayoelekeza utoaji wa Elimu bila malipo kama moja ya ahadi ya Mheshimiwa Rais Magufuli wakati wa kampeni za mwaka 2015, kwa maana hiyo Elimu bila malipo ilianza rasmi mwaka 2016 ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Sera hiyo ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 imetamka kuwa Serikali itahakikisha Elimu msingi (Elimu ya Awali hadi Kidato cha Nne) inakuwa ya lazima na bure kwenye Shule za Umma.
Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Ufundi ilitoa Waraka wa Elimu namba 5 wa Mwaka 2015 ambao unafuta ada kwa Elimu ya Sekondari kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne kwa Shule za Umma na michango yote katika Elimu msingi, hivyo basi, Waraka huu unafuta Waraka namba 8 wa Mwaka 2011 kuhusu michango Shuleni.
Aidha, Waraka huo wa Elimu namba 5 unafafanua kuwa ‘Serikali imeamua kutoa Elimu msingi (kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Nne) bila malipo. Azma hii ya Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ambayo ina lengo la kuhakikisha kwamba Watoto wa Kitanzania wenye rika lengwa la Elimu msingi wanapata elimu bila kikwazo chochote ikiwemo ada au michango’
Kuanza kwa utekelezaji wa Elimu msingi bila malipo, Manispaa ya Ilala kupitia Idara ya Elimu Msingi imefanya jitihada mbalimbali za kuboresha Sekta hiyo ili kutoa wigo mpana wa upatikanaji wa Elimu iliyo bora kwa kuboresha Mazingira ya kujifunzia kwa Wanafunzi kwa maana ya kuongeza nyenzo muhimu katika Miundombinu na Samani kama vile vyumba vya Madarasa, Matundu ya vyoo, Ofisi na Madawati.
Uandikishaji wa Wanafunzi wa Shule za Awali
Idadi ya Shule za Awali za Serikali kwa Manispaa ya Ilala hadi kufikia mwaka 2019 zipo 116 na idadi ya Wanafunzi ni 12,834, huku Wanafunzi waliondikishwa kwa kipindi cha miaka Minne kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 ni kama ifuatavyo; mwaka 2016 wanafunzi 8,905, mwaka 2017 wanafunzi 10,265, mwaka 2018 wanafunzi 10,051 na mwaka 2019 ni wanafunzi 12,834
Kuongezeka kwa uandikishaji Wanafunzi darasa la Kwanza
Ni ukweli usiopingika kuwa Elimu ya Msingi ni moja kati ya nguzo muhimu ya kujenga maarifa kwa Jamii ili kuchochea maendeleo na kutimiza azma ya Serikali ya Rais Magufuli ya kuhakikisha hakuna mtoto ambaye anafikia rika lengwa anashindwa kwenda shule.
“Kwa miaka Minne sasa, tangu mwaka 2016 hadi 2019 hali ya uandikishaji wa Wanafunzi wa darasa la kwanza imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka kufuatia uamuzi wa Serikali kutekeleza Elimu Msingi Bila Malipo (Waraka Na.3 wa mwaka 2016) Idara ya Elimu Msingi Manispaa ya Ilala, imeandikisha Wanafunzi wengi zaidi tofauti na makadirio ya awali, mfano mwaka 2016 maoteo yalikuwa ni Wanafunzi 19,705 waliokuja kuandikishwa darasa la kwanza ni 26,325 sawa na 133.6%, mwaka 2017 maoteo yalikuwa 27,019 waliondikishwa ni 25,425% sawa na 94%, mwaka 2018 maoteo yalikuwa ni 21,662 walioandikishwa ni 31,634 sawa na 146% na mwaka 2019 maoteo yalikuwa ni 25,393 walioandikishwa ni 30,867 sawa na 120%” Bi. Elizabeth Thomas, Afisa Elimu MsingiManispaa ya Ilala.
Sambamba na uandikishaji huo, lakini pia idadi ya jumla ya Wanafunzi wa Shule za Msingi za Serikali imekuwa ikiongezeka kama ifuatavyo; mwaka 2016 idadi ya Wanafunzi ilikuwa ni 163,903 mwaka 2017 wanafunzi walikuwa ni 176,987 mwaka 2018 wanafunzi walikuwa ni 176,680 na mwaka 2019 idadi ya wanafunzi imekuwa 186,393.
Kwa kuangalia takwimu za uandikishaji wa Wanafunzi wa darasa la Kwanza kwa Shule za Msingi za Manispaa ya Ilala, tunaanza kuona mafanikio makubwa katika sekta ya elimu katika jitihada za Serikali kufuta ujinga pamoja nakutekeleza Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs), kwani Elimu bila malipo imetoa fursa kwa watoto wengi walikuwa wakiikosa kutokana na gharama ikiwemo ada na michango mbalimbali kuondolewa.
Uboreshaji wa Miundombinu na Samani
Ongezeko la Wanafunzi limeleta chachu kwa Idara ya Elimu Msingi Manispaa ya Ilala na kupelekea kufanyika jitihada mbalimbali ili kukabiliana na hali hiyo, jitihada hizo ni pamoja na kuanzisha kampeni maalum za kuchangia elimu kwa kushirikisha Wadau mbalimbali wa elimu, huku kampeni hizo zikianzia ngazi ya Wilaya, Mkoa na Kitaifa.
Mpango wa ugawaji wa Madawati uliozinduliwa na Mheshimiwa Rais Magufuli Julai 13, 2016 kutoka kwenye fedha iliyobanwa matumizi ya Bunge ulizidisha hamasa ya kampeni ya uchangiaji Madawati kwa Manispaa ya Ilala hivyo kufanikisha upatikaji wa Madawati 22,403 kati ya hayo Madawati 1,694 yalitoka katika Mfuko wa Jimbo (Majimbo matatu ya Ilala, Ukonga na Segerea). Isitoshe Madawati 2,282 yalitoka kwa Wafadhili ambao ni PEPSI, EWURA, TRA, CRDB, NMB, Jamani Foundation na wengineo. Madawati 1,611 yamepatikana kutoka Serikali Kuu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Ilala Mh. Idd Azzan Madawati yaliyotolewa na Ofisi ya Bunge kwa niaba ya Wabunge waliopata mgao huo katika awamu ya kwanza
“Tumefanya uboreshaji mkubwa katika eneo la Miundombinu na Samani katika Shule zetu kwa kushirikiana na Serikali kuu na wadau mbalimbali wa Elimu, kama isemavyo ibara ya 52 ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inayoelekeza kuimarisha mazingira bora ya kufundishia na kuendelea kuimarisha miundombinu ya shule kama madarasa, vyoo, ujenzi wa nyumba za Walimu na madawati” Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala Bi. Elizabeth Thomas
Aidha, katika kipindi cha 2015/2016-2018/2019 Halmashauri imendelea kuboresha mazingira ya utolewaji wa elimu kwa kujenga Madarasa 224, yenye thamani ya TSh. 3,109,000,000/= ujenzi wa matundu ya vyoo 262 yenye thamani ya TSh. 515,010,300/= umaliziaji wa nyumba 3 za Walimu zenye thamani ya TSh. 75,000,000/= ukarabati wa shule kongwe 10 zenye thamani ya TSh. 258,465,150/= ujenzi wa shule mpya 8 zenye thamani ya TSh. 520,000,000/= na ununuzi wa madawati 7,125 yenye thamani ya Tsh 754,562,500 yote hayo yamefanyika kwa mapato ya ndani (own source)
Sambamba na hilo, lakini pia kupitia fedha za Ruzuku, Halmashauri imejenga madarasa 26 yenye thamani ya TSh 468,602,189/= Matundu ya vyoo 45 yenye thamani ya TSh 71,268,823/= ujenzi wa Shule mpya 2 zenye thamani ya TSh 468,000,000/= umaliziaji wa maboma 18 kwa TSh 225,000,000/= na ukarabati wa shule 4 kwaTsh 366,612,353/=.
Pia katika kipindi cha 2015/2016- 2018/2019 Halmashauri imepokea fedha kwa ajili ya elimu bila malipo na fidia ya ada jumla ya TSh 4,858,641,260/=
Kupandisha Viwango vya Ufaulu
Kasi ya ufaulu kwa Shule za Manispaaya Ilala imekuwa kubwa kwa kipindi cha miaka minne, hi inikutokana ushirikiano uliopo kuanzia kwa Walimu, Wazazi/Walezi hadi kwa Viongozi.
“Kwa ujumla matokeo ya Mtihani wa kumaliza Elimu Msingi na Upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne ni mazuri sana, kwani asilimia za ufaulu zimekuwa zikipanda mwaka hadi mwaka, mfano matokeo ya Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2016 hadi 2018 yalikuwa yakipanda kama ifuatavyo; mwaka 2016 tulishika nafasi ya 17 Kitaifa, na ufaulu wa 81.54%, mwaka 2017 tukapandisha ufaulu kwa kupata 92.46% ikiwa nitofauti ya 10.92% ya mwaka 2016 nakushika nafasi ya 4 Kitaifa, mwaka 2018 tulishika tena nafasi ya 4 Kitaifa kwa ufaulu wa 95.59% ikiwa ni ongezeko la 3.13% tofauti na ufaulu wa mwaka 2017” Bi. Elizabeth Thomas, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala.
Aidha, matokeo ya upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne na yenyewe yamekuwa yakipanda kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2016 hadi 2018, ambapo mwaka 2016 tulishika nafasi ya 7 Kitaifa kwa ufaulu wa 95%, mwaka 2017 tulishika nafasi ya 17 na ufaulu wa 98.97% ikiwa niongezeko la 3.97% tofauti na mwaka 2016, mwaka 2018 tulishika nafasiya 4 na ufaulu wa 99.56% ikiwa niongezeko la ufaulukwa 0.59% ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2017.”
Maktaba mpya iliyojengwa Shule ya Msingi Gogo, imesaidia kuongeza ufaulu Shuleni hapo