Manispaa ya Ilala yapitisha Bajeti ya Shilingi Bilioni 181.7 kwa mwaka wa fedha 2020/2021

Na: Hashim Jumbe
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, leo limefanya kikao maalum cha mapitio ya Bajeti ya mwaka 2019/2020 na mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 wenye Jumla ya Shilingi Bilioni 181.7, ambapo kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 60 sawa na 33.02% ya Bajeti yote ni kutoka kwenye vyanzo vya Mapato ya ndani na Shilingi Bilioni 121.7 sawa na 66.9% ya Bajeti ni ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Aidha, Bajeti ya Mapato ya ndani ya mwaka 2020/2021 imeongezeka kwa 5% ukilinganisha na Bajeti ya Shilingi Bilioni 57 ya mwaka 2019/2020, hii imetokana na kuongezeka kwa gharama za uchangiaji huduma za afya pamoja na uwepo wa hospitali mpya ya Wilaya Kivule inayotarajiwa kuanza kutoa huduma hivi punde, ambapo itaongeza mapato sambamba na kituo cha afya cha Mzinga, Zahanati ya Lubakaya, Bangulo, Luhanga na Mbondole.

Katika kuandaa Mpango na Bajeti ya mwaka 2020/2021 Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imezingatia Mwongozo wa uandaaji wa bajeti uliotolewa na Hazina mwaka 2019, Ilani ya CCM ya mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, hotuba ya Rais Magufuli ya Novemba 2015, Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015, Vipaumbele vya Halmashauri na Maoni ya Wadau mbalimbali.

Aidha, katika makisio ya mpango na bajeti ya mwaka 2020/2021 Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imejiwekea vipaumbele kumi na moja (11) huku ikiwa na mikakati saba (7) katika kufanikisha utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2020/2021.

Matumizi ya Mapato ya ndani
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa mwaka 2020/2021 kwenye Mapato yake ya ndani inatarajia kutumia fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 60 katika mchanganuo ufuatao;
Ø Matumizi mengineyo Shilingi 16,083,233,280 sawa na 26.8%
Ø Mishahara Shilingi 2,311,166,720 sawa na 3.8%
Ø Miradi ya Maendeleo Shilingi 27,591,600,000 sawa na 45.9%
Ø Mapato ya vyanzo fungiwa Shilingi 14,014,000,000  sawa na 23.3%

Makisio ya fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu
Ruzuku ya Shilingi Bilioni 121.7 kutoka Serikali imegawanywa katika maeneo mawili ambayo ni; Matumizi ya kawaida na Miradi ya Maendeleo.

Mchanganuo wa Matumizi ya kawaida kwa fedha za ruzuku
Ø Mishahara Shilingi 91,024,147
Ø Matumizi mengineyo (OC) Shilingi 2,116,869,000

Mchanganuo wa fedha za Miradi ya Maendeleo kwa fedha ya ruzuku
Ø DMDP  TSh. 18,228,375,100
Ø Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya TSh. 500,000
Ø Ujenzi wa Miradi Mkakati TSh. 2,500,000,000
Ø Mfuko wa Jimbo 189,180,000
Ø Capitation Grants-Dev 1,868,149,000
Ø School fees compensation grants 1,102,710,000
Ø Responsibility grants 546,600,000
Ø School meals grants 830,843,000
Ø Health sector basket fund 2,865,701,325


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi