Uongozi
ni mamlaka au karama anayopewa mtu kuwaonyesha watu njia kwa vitendo. Kipimo
cha uongozi ni namna ambavyo kiongozi anaweza kuleta ushawishi kwa watu na
kufikia maendeleo yaliyotarajiwa.
Katika
matoleo ya jarida hili tutakuwa na mfululizo wa makala kuhusu uongozi kama
itakavyokuwa ikizungumziwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bw. Jumanne
Shauri. Hii ni sehemu ya kwanza ya makala hiyo;
Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala Bwana Jumanne Shauri anaanza kwa kuongelea namna ambavyo
kiongozi bora anatakiwa kuwa ili kufanikisha malengo yake anayoyapanga katika
kuhudumia watu anaowaongoza.
Akihojiwa
na mwandishi wa jarida hili Mkurugenzi amesema kiongozi lazima awe na dira
itakayo muwezesha kupanga mpango mkakati ili kukamilisha dira hizo kwani
viongozi waliofanikiwa hutengeneza dira
na kufanikiwa katika uongozi wao kupitia dira walizoziweka.
Dira ni nini?
Dira
ni kifaa cha kutambua mwelekeo hivyo dira inapaswa kuonesha muelekeo wa
kiongozi wapi alipotoka na ndoto anazotaka kuzifikia. Dira ndio nguzo kuu ya
kiongozi itakayo mwezesha kufanikisha malengo yake kupitia mipango ya kimkakati
atakayo iweka kwa kulinganisha dira yake na ndoto zake.
Na
sio tu kwa kiongozi bali mtu yoyote ili
afanikiwe malengo yake lazima awe na dira na ndoto ili apate muelekeo wa nini
anakitaka kukifikia na pia kutengeneza mikakati ya kufikia jambo lake. Katika
kuliongelea hilo Bwana Shauri alisema “hata wanafunzi wakitaka kufaulu masomo
yake lazima aweke dira kwamba anataka kufikia ufaulu gani mathalani ufaulu wa
daraja la kwanza kisha aweke mikakati ni namna gani anaweza kufikia mafanikio
hayo”.
Pia
Mkurugenzi anasema ” mtu huwezi kukurupuka tu na kusema leo unataka kukimbia
mbio za riadha kama hauna maandalizi hivyo ni lazima ujiandae kwa muda hata
miezi sita au ndani ya mwaka mmoja ndipo
uweze kushiriki riadha na kufanikiwa kushinda”
DIRA ZA VIONGOZI TANZANIA
Tangu
awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi Tanzania, viongozi wake wote walikua na dira
waliozitumia katika kuhudumu muda wote wa uongozi wao na kufanikisha mengi kwa
kufuata dira hizo.
Tangu
nchi ipate uhuru mpaka sasa Tanzania ina awamu tano za uongozi na awamu zote
viongozi wake walihudumu kwa mafanikio makubwa kwa kutumia dira za maendeleo na
mipango ya kimkakati ya kufikia dira hizo
Awamu
ya kwanza ya uongozi Tanzania chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
ulikua na dira ya kupiga vita umasikini, maradhi na ujinga ili kuhakikisha kila
mtanzania anakua na maisha bora.
Dira
hiyo ilifanikiwa na kuwafanya wananchi kuondokana na ujinga kwa kufanya elimu
kuwa bure ili watanzania wote waweze kusoma hata kama wana hali ya umasikini.
Watoto pia walipata nafasi ya kufundishwa na walimu wa UPE na kupata elimu ya msingi iliyowasaidia kujua
kusoma na kuandika.mwalimu
Julius Nyerere aliamzisha elimu ya kujitegemea kuanzia shule za msingi mpaka
sekondari na vyuoni huku lengo la elimu hiyo likiwa ni kuondoa ujinga pamoja na
kuwafanya watanzania wasiwe wageni wa mazingira yao na kuyatumia vyema ili
kuweza kujiingizia kipato kwa shughuri mbalimbali za kiuchumi kama kilimo,
uvuvi pamoja na useremala.
Katika suala la kuondoa umasikini
Mwalimu Nyerere alianzisha taasisi ya chakula na lishe. Mapema
kabisa wakati Dunia ikiwa bado haijui mchango wa lishe bora kwa watoto na hapa
Afrika Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kabisa kuanzisha kituo maalumu cha
kutafiti na kuishauri serikali juu ya lishe ya watoto na watu wake kwa ujumla
(Tanzania Food and Nutrition Centre). Mpaka leo Tanzania inaheshimika duniani
kote kwa kuwa na wataalamu wabobezi katika lishe. Mataifa mengi duniani kote
huja hapa nyumbani kujifunza namna kituo chetu cha chakula na lishe
kinavyochagiza mipango makini ya afya ya ulaji serikalini na kwa wananchi
Mkurugenzi
Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Mseru amewahi
kusema kuwa mwalimu Julius Nyerere ndio muasisi wa bima ya afya ya jamii mwaka
1962.Profesa Mseru ameeleza hayo Oktoba 11, 2019 wakati akizungumza katika
kongamano la siku mbili la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na
taasisi ya uongozi kwa ushirikiano na UDSM. Amesema japo Serikali wakati
huo hakikuwa kubwa kama sasa, lakini Nyerere alijua mahitaji ya wananchi
na changamoto wanazozipata katika
matibabu yao kwa kutokuwa na utaratibu huo. .
Lakini
pia katika kupigana vita na adui umasikini mwalimu julius kambarage Nyerere alianzisha falsafa ya ujamaa na kujitegemea
lengo kuu la falsafa hii lilikuwa ni kulifanya taifa la Tanzania kuwa na uchumi
wa kujitegemea na kutokuwa ombaomba kwa mabeberu. Kufuatia dhima hiyo mwalimu
nyerere alikuja na mipango mkakati mbalimbali ya kuhakikisha sera ya ujamaa na
kujitegemea inaikia malengo kwa kumfaidisha kila mtanzania ambapo alianzisha
mipango mbalimbali ikiwemo mashamba ya vijiji, pamoja na kuanziaha viwanda ili
kuwezesha upatikanaji wa ajira miongoni mwa watanzania ili kuweza kupata kipato
cha kujikimu kimaisha.
kwa upande wa Rais Mstaafu wa awamu
ya pili Mhe. Ally Hassan Mwinyi alikuja na Dira ya kuikomboa nchi katika hali
mbaya ya kiuchumi ya nchi yetu kutokana na athari ya vita ya Kagera wakati huo
hiyo kuja na kauli mbiu ya RUKSA. Dira hiyo iliangazia kupigania
wanyonge na watu wa hali ya chini kwani alitoa ruksa kwa shughuli zote halali
zilizokatazwa kufanywa kufanyika bila kuvunja sheria za nchi. Dira hiyo
ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Rais wa awamu ya tatu Hayati
Benjamin Mkapa yeye aliongoza Tanzania chini ya Sera ya ubinafisishaji akilenga
Taifa la Tanzania liweze kuingia katika uchumi wa kati katika maendeleo yake.
Akiwa madarakani Rais Mkapa alibinafsisha baadhi ya mashirika yanayomilikiwa na
Serikali na akatumia sera ya soko huru. Dira yake ilipata msaada wa Benki ya Dunia
na shirika la fedha duniani IMF na kuwezesha baadhi ya madeni ya nje ya
Tanzania kufutwa. Aidha Mhe. Mkapa alifanya juhudi za kupambana na ufisadi
zilizopelekea kuundwa kwa jukwaa la wazi lililoitwa Tume ya Rais juu ya ufisadi
iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba na kuongeza msaada katika
mapambano hayo.
Awamu
ya nne ya Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ilikuja na dira ya maisha bora kwa kila
mtanzania kwa kuzingatia anapitia na kuboresha kila sekta ili watanzania wote
wanufaike na nchi yao kwa kuwa na maisha bora kwanzia daraja la juu mpaka
wananchi wa daraja la chini. Mipango hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani
watanzania wengi maisha yao yalibadilika na kuwa bora. Maboresho yalifanyika kwenye sekta ya ulinzi
na usalama, huduma za kijamii na sekta ya utalii pamoja na uwekezaji sekta nyengine muhumu
zenye kuleta maendeleo chachu kwa maisha bora ya watanzania.
Rais wa awamu ya tano wa Jamuhuri ya Muungano
wa tanzania Dkt John Pombe Magufuli kupitia sera ya HAPA KAZI TU ametekeleza
dira alizoziweka tangu aanze kuhudumu katika kipindi chake na kuhakikisha dira
zilizowekwa na Maraisi wa awamu zilizopita zinafikiwa kikamilifu.
Katika
kukamilisha sera na dira yake Rais Magufuli anaamini kwamba viwanda vitakua
nguzo katika taifa ili kuleta uchumi ulio bora huku ukitengeneza ajira kwa
Watanzania wengi. Rais Magufuli amezidi kujikita katika misingi ya baba wa Taifa
katika kujenga vituo vingi vya afya ili kutokomeza adui ambae ni maradhi,
kaboresha shule nyingi na kujenga na ameweza kutekeleza sera ya Elimu Bure ili
kila mtoto wa kitanzania aweze kusoma.
Sambamba na hayo Shauri aliongelea
Viongozi wakubwa Duniani ambao walikua na dira katika uongozi wao
zilizosababisha kufikia mafanikio viongozi hao ni pamoja na Mao Zedong wa China, Mahatma Gandhi wa India na Martin Luther King wa
Marekani.
Mahatma
Gandhi alikuwa mwanasheria, mwanafalsafa na mtetezi wa haki za binadamu na
kiongozi wa juu wa siasa nchini India.Ghandi alifanya kazi kwenye shamba la
miwa nchini Afrika Kusini lakini aliweka
dira kwamba akirudi nchini kwake atahakikisha India inapata uhuru. Aidha
aliporejea India aliweka mipango ya kimkakati kwa kutumia mbinu ya uasi wa
kiraia usio wa vurugu ulioisaidia india kupata uhuru na kuhamasisha mavuguvugu
kadhaa ya haki za kiraia na uhuru Duniani.
Naye
Mao Zedong alikua ni kiongozi wa Jamhuri ya watu wa China kuanzia mwaka 1949 na kiongozi wa chama cha
kikomunisti cha China tangu 1935 hadi kifo chake 1976. Katika hatua za mwanzo siasa
yake ya kiuchumi ilisababisha njaa na vifo vingi wakati wa utekelezaji lakini maono
na ndoto za Mao zilikua ni kuipeleka China katika uchumi ambao sasa tunauona. China
imekua nchi ambayo ina uchumi wa juu kutokana na sera iliyowekwa na Mao.
Martin Luther King alikua na dira na ndoto kuwa ipo
siku moja Marekani itaongozwa na mtu mweusi na ndoto hiyo ilitimia kwani mnamo
mwaka 2009 hadi mwaka 2017 Nchi ya marekeni iliongozwa na mmarekani mweusi Barack
Hussein Obama akiwa kama raisi wa awamu ya 44 kupitia chama cha Democratic.
HITIMISHO
Katika kuhitimisha sehemu hii ya
kwanza ya makala Mkurugenzi Jumanne Shauri ametolea mfano jinsi kiongozi wa Taifa letu Dkt. John
Pombe Magufuli ametekeleza Dira kwa vitendo baada ya kuahidi kufika kwenye
uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025 na
hatimaye kufikia malengo hayo ndani ya mwaka 2020, na kusema kuwa hayo yote
yamewezakana ndani ya muda mfupi kutokana na ukweli kuwa kiongozi wetu wa
Nchi alipoingia tu madarkani aliingia na
sera yake ya HAPA KAZI tu na kuja na mipango ya kimkakati ya kutimiza sera hiyo
kwa kuanzisha na kufufua viwanda ili kutoa fursa ya ajira kwa kila mtanzania.
Aidha
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Jumanne Shauri amezishauri Manispaa kuwa zinaweza
kuweka dira ya kujitegemea na kujiendesha kwa mapato binafsi kwani mpaka sasa
kuna baadhi ya Manispaa zinajiendesha zenyewe kwa zaidi ya asilimia ishirini
(20%) hivyo wanaweza kuweka dira ya
kujitegemea kwa zaidi ya hapo.