Madiwani Jiji la DSM wafanya uchaguzi wa Naibu Meya pamoja na kupitisha ratiba za vikao vya Kamati za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 04 Oktoba, 2023 limefanya Kikao Maalumu katika Ukumbi wa Arnatouglou cha kumchagua Naibu Meya wa Jiji la DSM ikiwa ni kutekeleza kanuni za uchaguzi wa Naibu Meya ambao hufanyika kila baada ya mwaka mmojaambapo katika uchaguzi huo Mhe. Ojambi Masaburi ambaye ni Diwani wa Kata ya Chanika amepita tena kwa kishindo baada ya kupata kura 45 sawa asilimia 100 ya kura zilizopigwa.


Akiongea baada ya ushindi huo, Mhe. Masaburi alitoa shukrani za dhati kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Waheshimiwa Madiwani wote kwa kuendelea kumuamini na kumpigia kura hivyo kuahidi kushirikiana nao katika kuwatumikia wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kuwaletea maendeleo.


Akitoa salamu zake kwa Baraza la Madiwani baada ya Uchaguzi huo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amempongeza Naibu Meya kwa kuchaguliwa tena kwani hii inaonesha wajumbe wameamini kazi alizozifanya na kuziomba Kamati ya Fedha pamoja na Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii kuhakikisha wanasimamia miradi ya Maendeleo kwa ukaribu zaidi huku akiwataka kufanya ziara katika shule za Sekondari Ari pamoja na Bangulo lengo likiwa ni kuzifanyia tathmini shule hizo hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao katika kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.


Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomaary Satura amewataka wajumbe wa Baraza kuhakikisha wanasimamia miradi ya Maendeleo vizuri lengo likiwa ni kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inabaki katika uimara wake kwenye ukusanyaji wa mapato na usimamizi mzuri wa Miradi ya Maendeleo.


Aidha kikao hicho kiliambatana na uundaji wa Kamati za Kudumu za Halmashauri pamoja na uchaguzi wa Wenyeviti wa Kamati hizo ambapo Mhe. Saady Khimji akichaguliwa kuwaMwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii huku Kamati ya Mipango Miji na Mazingira Mwenyekiti akiwa Mhe. Nyansika Getama na Mhe. Saada Mandwanga akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili.


Akifunga kikao hicho Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto aliwaasa Waheshimiwa Madiwani na Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuvumiliana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.


Katika Kikao hicho Baraza liliweza kupitisha ratiba za vikao vya Kamati za Kudumu zaHalmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi