RC Chalamila Aridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila aridhishwa na matumizi ya fedha na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Fedha toka Serikali Kuu pamoja na fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.


Hayo ameeleza leo tarehe 20 Novemba, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimlbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.


Miradi iliyotembelewa na Mkuu wa Mkoa ni pamoja ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Mvuti inayotekelezwa kwa fedha kutoka Mradi wa Kuboresha ubora wa elimu ya shule za sekondari (SEQUIP) kiasi cha shilingi milioni 528.9 mradi ukiwa hatua mbalimbali za ukamilishaji wa madarasa 8, maabara 3, Jengo 1 la Utawala, maktaba 1, Jengo la TEHAMA, kichomea taka na matundu 8 ya vyoo, ujenzi wa Zahanati ya Nzasa wenye thamani ya shilingi milioni 150 ujenzi ukiwa umekamilika katika jengo la OPD pamoja na RCH huku ujenzi wa mfumo wa maji taka ukisubiri ujenzi wa mashimo pamoja na ujenzi wa ngazi ndipo mfumo huo uanze kutekelezwa.


Akizungumza na wananchi baada ya kukagua mradi wa Shule ya Sekondari Mvuti Mhe. Chalamila amesema ili kuacha alama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuwekeza nguvu zaidi katika sekta ya elimu na Afya ili wananchi wapate huduma bora kwa ukaribu zaidi na kwa wakati.


Nipende kutoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha kwaajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini ambapo katika shule mpya ya Mvuti mmepewa takribani shilingi milioni 528.9 kwaajili ya ujenzi wa shule hii hivyo nimpongeze Mkuu wa Shule pamoja na wataalamu wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa usimamizi mzuri wa mradi huu ambao thamani ya fedha iliyotumika inaendana na mradi wenyewe hivyo niwaombe muendelee kusimama vyema miradi mingine inayotekelezwa kwa kuiga mfano wa shule ya Mvuti Mpya pia muhakikishe mfumo wa maji taka katika Zahanati ya Nzasa unaanza utekelezaji na mifereji ya maji ijengwe ili maji yasiweze kutuama.


Sambamba na hilo RC Chalamila amesema katika kipindi hichi cha mvua hakuna eneo lolote la Mkoa huo lililoripotiwa kuwa na mafuriko, ingawa miundombinu ya barabara imeharibika na kumuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala kuhakikisha mvua zikikata aungane na wataalamu kutembelea maeneo yaliyoadhiriwa na mvua ili yaweze kufanyiwa marekebisho ya muda mrefu huku akisisitiza kipindi hichi cha mvua barabara zisifanyiwe marekebisho ya muda mfupi ambayo yataleta athari zaidi bali ikitokea eneo hilo linastahili marekebisho ya muda mfupi lifanyiwe marekebisho huku akiwataka wazazi kuwaangalia watoto wao kwa ukaribu zaidi kipindi hichi cha mvua ili kuepukana na athari zinazojitokeza.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ametoa shukurani zake kwa Mkuu wa Mkoa kwa Ziara aliyoifanya ya kukagua miradi ya Maendeleo pamoja na kuongea na wananchi huku akimuhakikishia kutekeleza yote aliyoyaagiza.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi