Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo leo Februari Mosi, 2024 amekabidhi vifaa saidizi kwa walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili viwasaidie katika utendaji kazi pamoja na kuchochea maendeleo ya Wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika ufaulu pamoja na kuimarisha Sekta ya Elimu Maalumu kwa ujumla ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Akiongea kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika kwenye Shule ya Msingi Uhuru Wasichana, Mhe. Mpogolo ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada wa vifaa hivyo na kusema lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote wanapata elimu iliyokusudiwa pamoja na kuweka usawa kwa makundi yote ya kijamii katika ngazi zote.
"Tunawashukuru sana Benki ya NMB kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha elimu nchini. Vifaa hivi vitaenda kuimarisha ujifunzaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kuondoa vikwazo vilivyokua vinasababisha wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo wakati wote."
Naye Afisa Elimu Sekondari Mwl. Mussa Ally akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, amesema Halmashauri ya Jiji la DSM itaendelea kuweka mkazo kwenye elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuboresha miundombinu mashuleni pamoja na kununua vifaa saidizi kwa lengo la kukabiliana na vikwazo dhidi ya uwepo ushiriki na ujifunzaji kwa wanafunzi hao.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na fimbo nyeupe sitini (60) kwaajili ya wasioona, lensi sitini (60) kwaajili ya wenye uoni hafifu, kofia sitini (60) na mafuta chupa sitini (60) kwa wenye ulemavu wa ngozi na vifaa hivyo vitagaiwa kwa walimu na wanafunzi wenye ulemavu wa shule za msingi na sekondari.