Elimu ya Lishe yatolewa kwa vijana wa rika balehe wa shule za msingi na sekondari

Katika kuendeleza dhamira yake ya kuhakikisha Elimu ya Lishe inatolewa katika maeneo yote na watu wa rika zote, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea na utoaji wa elimu ambapo leo tarehe 20 Februari 2024 imetoa elimu kwa vijana wa rika balehe wenye umri kuanzia miaka 10 mpaka 19 wa Shule za Msingi Mnazi Mmoja na Gerezani pamoja na Shule ya Sekondari ya Dar es Salaam.


Akiongea wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Kaimu Mratibu wa Lishe wa Jiji la DSM Bi. Neema Mwakasege amesema lengo la elimu hii ni kuhakikisha vijana wa rika balehe wanakua na afya bora.


"Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kuimarisha na kuwekeza kwenye afya za vijana wa rika balehe kama ilivyoainishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe namba 2 wa mwaka 2021/2022 - 2025/2026 ambapo vijana rika balehe wamepewa kipaumbele kutokana na changamoto wanazozipata za uzito mkubwa, uzito mdogo na ukosefu wa vitamini na madini." Ameeleza Bi. Mwakasege.


Aidha, wanafunzi hao walipewa elimu mbalimbali kuhusiana na lishe ambapo Afisa Lishe Bi. Neema Manyama alitoa masomo juu ya Umuhimu wa kula mlo kamili kutoka makundi sita ya vyakula, ambayo ni :- 

1. Vyakula vya kuupa mwili nguvu vinavyojumuisha vyakula vya nafaka, mizizi, ndizi mbichi na mbogamboga

2. Vyakula vya kuupa mwili vitamini na kulinda mwili na magonjwa 

3. Kundi la matunda ambalo husaidia mwili kupata madini na afya bora

4. Vyakula vya Jamii ya mikunde, jamii ya karanga na mbegu za mafuta kwaajili ya kujenga mwili

5. Vyakula vya asili ya wanyama kwaajili ya kujenga na kukarabati seli za mwili 

6. Mafuta, asali na sukari kwa kiasi kidogo ili kuupa mwili joto na nguvu


Naye, Bi. Happy Kanda ametoa elimu kuhusu mtindo bora wa maisha kwa kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi ya mwili kila siku angalau kwa dakika 30, kuepuka msongo wa mawazo na uvutaji wa bidhaa zitokanazo na tumbaku.




Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi