Jiji la DSM lapitisha Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Tshs. Bilioni 278 kwa mwaka 2024/25

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo Tarehe 20 Februari, 2024 limefanya Mkutano Maalum wa Mapitio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2023/2024 kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai-Desemba, 2023) na kufanya Makadirio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 wenye Jumla ya Tshs. Bilioni 278, ambapo kati ya fedha hizo kiasi cha Tshs. Bilioni 130 sawa na 47% ya Bajeti yote ni makusanyo kutoka vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri na Shilingi Bilioni 148 sawa na 53% ya Bajeti ni fedha za Ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Aidha, kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Arnatouglou na kuongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto, kilipokea, kikajadili na kisha kupitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo Bajeti hiyo imekua na ongezeko la jumla ya Tshs. Bilioni 40.9 sawa na 46% kutoka katika mapato ya ndani ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24, hii imetokana na mikakati bora iliyowekwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye ukusanyaji wa mapato na uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato.


Katika Makadirio ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2024/2025 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweka vipaumbele vitano (05) vitakavyolenga kutatua changamoto kwa ustawi wa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam

Akisoma taarifa kuhusu makadirio ya mpango na bajeti ya mwaka 2024/2025 mbele ya Baraza la Madiwani, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, Bw. Julius Ndele alisema "Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kukusanya Shilingi Bilioni 130 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani."


Matumizi ya Mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka 2024/2025

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwenye mapato yake ya ndani inatarajia kutumia fedha kiasi cha Tshs. Bilioni 130 katika mchanganuo ufuatao; Matumizi ya kawaida Tshs. Bilioni 21.3 sawa na 16.3%% ya Bajeti, Miradi ya Maendeleo Tshs. Bilioni 74.4 sawa na 57.2% ya Bajeti, Mishahara Tshs. Bilioni 2.2 sawa na 1.6% na Vyanzo Fungiwa Tshs. Bilioni 31.9 sawa na 24.5% ya mapato ya ndani.

Ruzuku ya Tshs. Bilioni 148 kutoka Serikali Kuu imegawanywa katika maeneo mawili ambayo ni Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo


Mchanganuo wa Matumizi ya kawaida kwa fedha ya Ruzuku

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kutumia Tshs. Bilioni 122.4 ya fedha ya ruzuku sawa na 82.4% kulipa Mishahara na Tshs. Bilioni 1.2 sawa na 0.85% kwa ajili ya Matumizi Mengineyo


Mchanganuo wa Fedha za Miradi ya Maendeleo kwa fedha ya Ruzuku

Katika kipindi kijacho cha 2024/2025 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kutumia Tshs. Bilioni 24.3 kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambayo ni sawa na 16.4%.


Katika kuandaa Rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeandaliwa kwa kufuata na kuzingatia Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015, mwongozo wa maandalizi ya bajeti (PBG) ya mwaka 2024/25, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020-2025, Mpango mkakati wa Halmashauri (SP), Mpango wa maendeleo wa miaka mitano (5YDP III 2020/2021 – 2025/2026), Malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), Waraka wa Hazina namba 4 wa mwaka 2024 pamoja na maelekezo mahsusi ya viongozi mbalimbali wa Serikali katika Halmashauri yetu kwa nyakati tofauti.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi