Walimu Wakuu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wafanya ziara ya kimafunzo Shule ya Msingi Olympio

Walimu Wakuu 42 wa Shule za Msingi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo leo tarehe 15 Februari, 2024 wamefanya ziara ya kimafunzo katika Shule ya Msingi Olympio yenye lengo la kujifunza mbinu za kufundisha na masuala mengine muhimu yatakayowawezesha kupandisha kiwango cha ufaulu.


Akiongea katika mafunzo hayo, Afisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mwl. Joseph Bureta amesema wameichagua Shule ya Msingi Olympio kwani ni Shule ya Serikali inayofanya vizuri kitaaluma katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa na kumshukuru Mwalimu Mkuu kwa mapokezi mazuri.


Lengo la kuja shuleni hapa ni kujifunza namna ya kuongoza shule na namna ya kusimamia mikakati ya kuinua taaluma katika Wilaya ya Bagamoyo. Tumeona jinsi walimu wanavyojituma na kuwasimamia wanafunzi licha ya kuwa na wanafunzi wengi lakini hali ya mazingira ni safi na utulivu wa wanafunzi unaridhisha. Nina imani kwa elimu hii tuliyoipata hapa walimu nilioambatana nao wataitendea kazi na kuleta mabadiliko chanya ya kitaaluma katika Wilaya yetu na Mkoa wa Pwani." Amesema Mwl. Bureta


Aidha, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Olympio Mwl. Reuben Mduma Gadi amesema ”Tunayo furaha kuwakaribisha Walimu Wakuu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo waliokuja kujifunza baada ya kuona shule yetu ina mafanikio kitaaluma miaka mitatu mfululizo. Lakini sisi kama Shule ya Olympio tumepata mengi kutoka kwao ambayo yatatusaidia kuboresha zaidi ufundishaji kwenye shule yetu."


Sambamba na hilo amesema “Namshukuru Rais Wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani aametusaidia kuhakikisha miundombinu ya shule inakua katika hali nzuri na uhakika wa upatikanaji wa vitabu shuleni, na kusaidia kwenye ujenzi wa jengo la ghorofa. Pia namshukuru Mkurugenzi wa Jiji kua nasi bega kwa bega. Vile vile nawashukuru walimu wote kwa kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano." Ameongeza Mwl. Gadi.

Awali akitoa mafunzo, Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo amesema ili kuleta ufanisi zaidi, utoaji wa elimu shuleni hapo ni shirikishi ambapo hushirikisha walimu wa Taaluma, wakuu wa idara, wakuu wa Vitengo na wadhibiti ubora.



Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi