Madiwani Jiji la DSM wapatiwa mafunzo ya Bajeti

Waheshimiwa Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam Leo 14 Februari, 2024 wamepatiwa mafunzo ya bajeti ya mapato yanayokusanywa na Halmashauri ya Jiji la DSM yenye lengo la kupata uelewa wa pamoja juu ya matumizi ya fedha za Halmashauri.


Akiongea katika mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ilala, Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa Idara, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala Ndg. Said Sidde amesema “Ili Halmashauri yetu iweze kufanikiwa katika miradi mbalimbali inahitaji mambo matano ambayo ni weledi katika Usimamizi wa mapato, Usimamizi mzuri wa miradi kwa Madiwani na Chama, Uwajibikaji wa watumishi, mgawanyo mzuri wa fedha na pia mpango kazi. Hivyo niwaombe wote tusimame kwenye maeneo haya ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea."


Sambamba na hilo Ndg. Sidde amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la DSM kwa kuandaa mafunzo hayo, na kuwataka madiwani kuwa na ushirikiano na upendo katika kutekeleza miradi kwa maslahi ya wananchi wa Wilaya ya Ilala.


Aidha, Mstahiki Meya Mhe. Omary Kumbilamoto amesema “Miradi yote katika Halmashauri yetu inatekelezwa kwa usawa. Nimpongeze Mkurugenzi pamoja na Watumishi wote kwa kuendelea kusimamia miradi kwa ufanisi na kuhakikisha inaendana thamani ya pesa inayotolewa."


Awali akitoa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Jiji la DSM Jomaary Satura amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwa na uelewa wa pamoja na uwazi juu ya mapato na matumizi ya Halmashauri.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi