Kamati ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imefanya ziara ya ukaguzi wa maeneo ya wazi Kariakoo ambayo yako chini ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambapo imetembelea maeneo ya Mtaa wa Swahili na Mkunguni, Msimbazi na Jangwani (sabasaba) pamoja na Kongo na Msimbazi.
Akiongea katika ziara hiyo, Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ojambi Masaburi amesema "Kamati hii ni mahususi kwa kubainisha maeneo ambayo ni fursa na vitega uchumi vya Halmashauri, kwani Halmashauri yetu ina maeneo mengi ya wazi ambayo tukiyatumia vizuri katika uwekezaji yatasaidia kuingiza mapato katika Halmashauri yetu ambayo yatasaidia kuboresha miundombinu."
Aidha, Kamati imeagiza Halmashauri ya Jiji kuendelea kubainisha maeneo yote ya wazi ambayo yamechukuliwa na watu binafsi au makampuni bila kufuata utaratibu pamoja na kupata taarifa za mapato yanayokusanywa katika maeneo ya wazi ya Halmashauri.