Kamati ya Fedha na Utawala yafanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa kwa kipindi cha robo ya pili (Oktoba - Desemba 2023)

Kamati ya Fedha na Utawala Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imefanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa na Halmashauri hiyo kwa kipindi cha Robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 (Oktoba - Desemba) 2023) ambapo leo tarehe 23 Februari, 2023 imetembelea miradi minne (4) ikiwemo Hospitali ya Wilaya Kivule, ujenzi wa matundu ya vyoo Shule ya Sekondari Zingiziwa, ujenzi wa madarasa ya ghorofa Shule ya Sekondari Amani pamoja na Kituo cha Afya Kinyerezi.


Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala Mhe. Omary Kumbilamoto amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam fedha kwaajili ya ukamilishaji na uboreshaji wa miundombinu katika Kituo cha Afya Kinyerezi ambazo zitarahisisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wananchi wa maeneo ya mbali.


Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imewataka Wahandisi wa Halmashauri wanaosimamia miradi kuhakikisha miradi inatekelezwa kulingana na makisio ya gharama za ujenzi (BoQ) inavyoelekeza lengo likiwa ni kufanya kazi kwa usanifu na umakini mkubwa, pia kamati imeagiza Wakandarasi kumaliza Miradi ndani ya muda uliopangwa na kwa usahihi huku ikitoa angalizo kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kushirikiana na wataalamu wa ujenzi kuhakikisha wanatatua changamoto zilizojitokeza katika miradi hiyo kwani ubora wa miradi hiyo itasaidia idumu kwa muda mrefu na kuwapunguzia Wananchi wa maeneo ya jirani adha ya kwenda umbali mrefu kufuata huduma hizo za kijamii.


Ziara hiyo itafuatiwa na kikao cha kamati kitakachojadili taarifa za utendaji kazi kwa Idara na Vitengo wanavyovisimamia pamoja na kupitia na kujadili taarifa ya miradi iliyotekelezwa kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2023.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi