Kamati ya Mipango Miji Jiji la DSM yakagua Usafi wa Mazingira Viwandani pamoja na Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa kwa kipindi cha Robo ya pili (Oktoba-Desemba 2023)

Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo Februari, 2024 imefanya Ziara ya ukaguzi wa Upangaji Miji na Mazingira ikiwa ni sehemu ya majukumu ya Kamati hiyo kusimamamia matumizi bora ya ardhi kwa kuzingatia mpango wa matumizi ya ardhi (Master Plan) ya Jiji na kusimamia matumizi sahihi ya Miundombinu iliyopo pamoja na usafi wa mazingira, hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi pamoja na utunzaji wa Mazingira kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 (Oktoba–Desemba 2023.)


Kamati iliweza kutembelea kiwanda cha kamba cha Dar Rope kilichopo Kiwalani na Kiwanda cha kuchakata upya betri cha GAIA kilichopo Vingunguti lengo likiwa ni kukagua hali ya usafi wa Mazingira na usalama wa wafanyakazi pamoja na Wananchi wanaozungukwa na viwanda hivyo.



Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Nyansika Getama akifanya majumuisho ya ziara hiyo amesema, “Leo tumetembelea baadhi ya miradi inayosimamiwa na kutekelezwa na Halmashauri ya Jiji la DSM ambapo tumeweza kuridhishwa na utekelezaji huo japo kuna marekebisho madogomadogo yakukamilisha hususani katika usalama wa wafanyakazi. Wafanyakazi wa viwandani watumie barakoa (mask) na gloves kwa usalama wa Afya zao."




Aidha, Kamati imeagiza wataalamu wa Divisheni ya Mazingira kuhakikisha viwanda vyote vinaboresha mazingira hasa vyoo vya wafanyakazi kwa usalama wa afya zao Ili kuepuka magonjwa ya mlipuko, na viwanda visivyofanya hivyo vipigwe faini kadri ya sheria na kanuni zinavyoelekeza.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi