Kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, Jiji la DSM lafanya maombi na dua ya kuliombea Taifa

Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 22, Aprili 2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imefanya Maombi na Dua ya kuliombea Taifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam yalioambatana na kaulimbiu isemayo “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleao ya Taifa Letu.


Akiongoza hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “Tumeandaa Maombi na Dua ya kuliombea Taifa letu ikiwa ni sehemu ya Kumshukuru Mungu kwa kufikisha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa amani kwani kama Taifa tumeshikamana na tumeimarika kwa miaka 60 hivyo hatuna budi kufanya Maombi na Dua kwaajili ya kuendelea kuimarisha amani ya nchi yetu.


Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo ameendelea kusema “Katika maombi na Dua hizi tunaendelea kumuombea Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuendelea kuimarisha Muungano kwa amani pamoja na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kupata maendeleo bila kusahau kuombea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaoenda kufanyika Oktoba 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 ufanyike kwa Amani na tupate viongozi bora zaidi watakaoendelea kutuletea maendeleo.


Kwa upande mwingine Mhe. Mpogolo amewahakikishia Wananchi wa Wilaya ya Ilala kutatua changamoto ya athari za mvua kwani tayari amewaelekeza wataalamu kutoka TARURA wakiambatana na Wahandisi kutoka Jiji la Dar es Salaam kutambua maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua ili pindi mvua zitakapopungua maeneo hayo yafanyiwe marekebisho.


Aidha, kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Jomaary Satura ameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa dini kuliombea Taifa letu huku akiwahakikishia kushirikiana na watendaji wake kutatua kwa wakati changamoto zinazowakabili wananchi wa Wilaya ya Ilala kama Mheshimiwa Rais anavyoelekeza.


Akitoa Shukrani zake kwa viongozi wa Dini walioshiriki kuliombea Taifa, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto ameeleza kuwa “Kupitia Maombi na Dua hizi za kuliombea taifa kufikisha Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Imani yangu maombi haya yatadumisha Amani na yatakuwa chachu ya maendeleo kwa nchi yetu."


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Sheikh wa Wilaya ya Ilala Adam Mwinyipingu ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuandaa siku ya Maombi na Dua ya kuliombea Taifa kwaajili ya Muungano kwani maombi haya ni sehemu ya uzalendo pamoja na mshikamano kwa viongozi huku akiahidi kusimama na kuimarisha Muungano wa Tanzania kupitia Dua na Sala ili nchi iendelee kuwa na amani.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi