Shilingi bilioni 10.75 kutekeleza Miradi ya Ujenzi wa Barabara Jiji la DSM

Shilingi bilioni 10.75 fedha kutoka mapato ya Halmashauri zimetengwa kwaajili ya ujenzi wa barabara Jiji la Dar es Salaam kwa kiwango cha lami na zege. Hayo yamebainishwa leo Julai 15, 2024 na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Jomaary Satura kwenye hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara 10 kati ya Jiji la Dar es Salaam na wakandarasi wanaoenda kutekeleza miradi hiyo.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka Wakandarasi kuwa waadilifu kwa kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati huku akiwasisitiza washirikiane katika kazi ili kuleta matokeo yenye tija kwa maslahi ya Wananchi.


Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo ametoa pongezi kwa Mstahiki Meya na Madiwani kwa usimamizi mzuri wa miradi huku akimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Watendaji wa Jiji kwa kasi ya ukusanyaji wa mapato ambao umekua chachu ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.


Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amemshukuru Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha anazotoa kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo huku akitoa wito kwa Wakandarasi kutekeleza miradi kwa wakati uliopangwa ilo waweze kutimiza adhma ya Rais ya kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.


Awali akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndugu Jomaary Satura ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imejipanga kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi kwa kuzingatia nyanja zote muhimu ikiwemo elimu, afya na miundombinu hivyo katika kutekeleza hilo JiJi la Dar es Salaam limeweza kutenga asilimia 10 za mapato ya ndani kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara ambapo bilioni 10.7 itatumika kutekeleza miradi hiyo.


Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tumekusanya shilingi bilioni 111 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 sawa na ongezeko la bilioni 30 ikilinganishwa na mwaka 2022/2023 hivyo kutokana na mapato haya kuongezeka, shilingi bilioni 10.7 imetengwa kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara 10 za ndani Jiji la Dar es Salaam zinazoenda kutekelezwa kwa kiwango cha lami na zege na leo tunasaini mikataba na wakandarasi wanaoenda kutekeleza miradi hiyo, hivyo niimani yangu wakandarasi waliochaguliwa ni wakandarasi wenye uwezo wa kujisimamia wenyewe na watakamilisha mradi kwa wakati pia niwatake muwe waadilifu kwa kutekeleza majukumu ipasavyo kwa faida ya watanzania wengine.” Amesisitiza Ndg. Satura.


Naye Mkandarasi kutoka Kampuni ya Southern Link Bw. John Mosha ameishukuru Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuchaguwa wakandarasi wazawa huku akiwahakikishia kutekeleza miradi hiyo kwa kiwango bora na kwa wakati.


Aidha, Miradi hii inatarajiwa kukamilika ndani ya muda wa miezi mitatu.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi