Walimu na Wanafunzi Shule ya Sekondari Juhudi wapongezwa

Diwani wa Kata ya Gongolamboto Mhe. Lucas Rutainurwa amewapongeza walimu wa Shule ya Sekondari Juhudi kwa juhudi wanazozifanya ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha sita kwa mwaka 2024.

Diwani wa Kata ya Gongolamboto Mhe. Lucas Rutainurwa (aliyesimama) akiongea na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Juhudi kwenye hafla ya kuwapongeza waliofanya vizuri kwenye mtihani wa kidato cha sita 2024

Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 19, 2024 wakati wa halfa ya kuwapongeza iliyoambatana na utoaji wa zawadi kwa walimu waliofaulisha masomo kwa daraja A na B na wanafunzi tisini na sita (96) waliopata daraja la kwanza (Division 1), iliyofanyika katika shule hiyo iliyopo Wilaya ya Ilala Jijini DSM.

Mmoja wa walimu Shule ya Sekondari Juhudi akipokea zawadi

Akiongea na walimu pamoja na wanafunzi hao, Mhe. Rutainurwa amesema "Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa shule. Pia nawapongeza walimu kwa jitihada zao kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu iliyokusudiwa, ufaulu umeongezeka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka iliyopita, hivyo walimu wanasikiliza na kutekeleza ushauri na maoni kutoka kwa viongozi na wazazi, ni kazi ngumu lakini hawakati tamaa, wazazi pia tusiache kufatilia maendeleo ya watoto wetu shuleni. Bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanafunzi wote wanafaulu na kuendelea na masomo ya juu hivyo niwaase kuendeleza jitihada hizi. Lakini pia natarajia walimu hamtabweteka na mtaongeza juhudi katika kufundisha ili wanafunzi wapige hatua kwenye suala la elimu na taaluma kwa ujumla."


Aidha, Mhe. Rutainurwa amewataka walimu kuwa na ushirikiano pamoja na malengo ya kufanya vizuri kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu ikiwa ni kuweza kubaini ni wapi wanafunzi wanakwama katika taaluma kabla yakufikia katika mitihani yao ya mwisho ya kuhitimu kidato husika.


Awali akifungua halfa hiyo Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Happiness Pallangyo amemshukuru Mhe. Rutainurwa kwa kushiriki katika halfa hiyo, na kusema halfa hii iwe chachu kwa wanafunzi wengine kufanya vizuri katika masomo na mitihani yao.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Juhudi (aliyesimama) Mwl. Happiness Pallangyo akiongea na wanafunzi kwenye hafla ya kuwapongeza waliofanya vizuri kwenye mtihani wa kidato cha sita 2024, halfa iliyoambatana na utoaji wa zawadi

"Hafla hii ni kwaajili ya kutambua juhudi na jitihada kubwa walizofanya walimu wetu kwenye mitihani ya kidato Cha sita mwaka 2024. Tunaamini tukio hili litaleta hamasa na chachu ya watu kujituma ili mwaka huu tuweze kufanya vizuri zaidi.

Lakini pia niwatake walimu mliopata zawadi kutobweteka badala yake muendelee kujituma Zaidi kwa maendeleo ya shule yetu." Ameongeza Mwl. Pallangyo.


Juhudi Sekondari ni shule iliyoongoza kwenye matokeo ya kidato cha 6 kwa Wilaya ya Ilala, mwaka 2024.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi