Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Jiji la DSM chaongezewa vifaa kuboresha Utoaji wa Taarifa

Katika kuhakikisha Halmashauri ya Jijj la Dar es Salaam inaendelea kuhabarisha Umma kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Jiji hilo leo Agosti 26, 2024 Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya amekabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi Milioni 36.4 kwa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikali lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa taarifa kwa Wananchi kwa kuhakikisha taarifa muhimu za utekelezaji wa Miradi zinawafiki kwa wakati.


Akikabidhi Vifaa hivyo kwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Ndg. Mabelya ameeleza kuwa “Lengo kubwa la Halmashauri yetu ni kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Jiji letu inafahamika kwa wananchi hivyo ni matumaini yangu vifaa hivi ninavyovikabidhi leo vitakwenda kuongeza nguvu katika kazi za kuhabarisha Umma pia niwahakikishie ushirikiano katika kuhakikisha tunaitangaza miradi inayotekelezwa katika Jiji letu ili wananchi waweze kuifahamu kwa ukaribu zaidi”.


Sambamba na hilo, Ndg. Mabelya ametoa pongezi kwa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini kwa kazi wanazozifanya huku akisisistiza kuendelea kuhakikisha habari za utekelezaji wa miradi zinawafikia Wananchi kwa wakati ili waweze kuifahamu miradi hiyo.


Awali akiongea wakati wa makabidhiano hayo Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Tabu Shaibu ameeleza kuwa “Tunamshukuru Mkurugenzi wetu kwa vifaa alivyotukabidhi leo kwani vifaa hivi vinaenda kuwa chachu ya kukibadilisha kitengo chetu kwa kufanya kazi zenye ubora zaidi hivyo tunaahidi ushirikiano na uboreshaji wa kazi zetu kwa kuhakikisha taarifa zote muhimu zinawafikia Wananchi kwa wakati pia tunakuhakikishia kufanya kazi kwa viwango unavyovitaka na tukuhakikishie vifaa hivi tutavitunza na kuvithamini”.


Naye Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bw. Selemani Kateti ametoa shukurani zake kwa Mkurugenzi wa Jiji kwa kununua vifaa hivyo ambavyo vitaenda kuwa chachu ya kirahisisha utoaji wa habari kwa Wananchi huku akitoa wito kwa watumishi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa wazalendo kwa kuifuatilia mitandao yote ya kijamii hii ikiwa ni kutambua kazi zinazofanywa na kitengo cha habari lakini pia ni njia nzuri ya wao kuitangaza Radio yetu ya City FM.



Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi