Watendaji Jiji la DSM wahimizwa kutengeneza mazingira wezeshi katika Ukusanyaji wa Mapato

Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamehimizwa kutengeneza mazingira wezeshi katika ukusanyaji wa mapato kwa kusimamia utaratibu pamoja na kuweka mazingira rahisi kwa wafanyabiashara ambao ndio wachangiaji wakubwa wa mapato kupitia kodi wanazotoa.


Hayo yamebainishwa leo Agosti 19, 2024 na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya wakati akikabidhiwa ofisi na Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji hilo Jomaary Satura ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke.


Aidha, Ndg. Mabelya amesisitiza ushirikiano na Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam huku akiwahakikishia kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kuwahudumia Wananchi lengo likiwa ni kutimiza adhma ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluh Hassan ya kuwahudumia wananchi kwa wakati na ukaribu zaidi.


Nipende kumpongeza Ndg. Satura kwa historia aliyoiweka katika ukusanyaji wa mapato, ninaamini tutashirikiana vizuri katika kutimiza majukumu ya Halmashauri kwa kuacha alama kama Mkurugenzi alivyoacha huku tukiwahudumia wananchi kwa ukaribu zaidi kwa kutekeleza na kuimarisha haya tuliyoyakuta hivyo Niombe ushirikiano wenu katika kuendelea kuimarisha Jiji letu.” Amesisitiza Mkurugenzi Mabelya.


Sambamba na hilo, Mkurugenzi Mabelya amehimiza kuimarisha mahusiano na Watumishi wa Jiji la Dar es Salaam huku akiwahimiza kujikita zaidi katika kutenda ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia Wananchi kwa ukaribu zaidi.


Awali Akimkabidhi Ofisi aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam ambaye kwa Sasa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Jomaary Satura ameishukuru Menejimenti ya Jiji la Dar es Salaam kwa ushirikiano waliomuonesha wakati wa Utumishi wake hususani eneo la ukusanyaji wa mapato.


Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amemshukuru Ndugu Satura kwa kazi nzuri aliyoifanya ya ukusanyaji wa mapato wakati wa utumishi wake akiwa Jiji la Dar es Salaam huku akiiahidi Ushirikiano kwa Mkurugenzi mpya katika kuendeleza yale yale yote yaliyokwisha kufanyika lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa ukaribu na kwa wakati zaidi.



Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi