TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UBORESHAJI WA UKUSANYAJI WA MAPATO
YA HALMASHAURI.
Katika
mwaka wa fedha wa 2014/15 Manispaa ya Ilala imepanga kukusanya jumla ya Sh.
30,000,000,000.00 kutokana na vyanzo
vyake vya ndani, ambapo kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2015 zimekusanywa Sh.
21,830,871,622.90 sawa na asilimia
73% ya lengo la mwaka. Katika
mwaka wa fedha wa 2015/16 tumepanga kukusanya Tshs. 58 bilioni.
Halmashauri
ya Manispaa ya Ilala iko katika hatua za kuboresha ukusanyaji wa mapato yatokanayo
na vyanzo vyake vya ndani. Hata hivyo kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa katika
vyanzo Vikuu vya ndani ambavyo ni vinne; Kodi ya Majengo, Leseni za Biashara,
Ushuru wa Mabango na Kodi ya Huduma za Jiji.
KODI
YA MAJENGO
Inatozwa
kutokana na sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1983 pamoja na
marekebisho yake na sheria ya uthamini ya kodi ya majengo ya mamlaka za miji
Urban Authority rating Act no. 2 ya mwaka 1983.Sheria hii inasisitiza kila jengo
litozwe kodi kiasi kisichopungua shilingi elfu kumi 10,000/=
Kuna
aina mbili za viwango vya tozo ya kodi za majengo. Nazo ni
Kodi
ya jengo la makazi asilimia 0.15 na Kodi ya majengo ya biashara asilimia 0.20
ya thamani ya jengo husika. Hivyo majengo yote yanayotumika kwa shughuli za
makazi na biashara yanatakiwa kulipiwa Kodi ya majengo. Kodi hii hulipwa mara
moja tu kwa mwaka. Kila mwaka Manispaa ya Ilala imekuwa ikiongeza kiwango cha
ukusanyaji wa kodi hii kutokana na ongezeko la majengo katika eneo lake. Ili
kuweza kutambua kiasi unachotakiwa kulipa kwa ajili ya jengo lako.Inasisitizwa
kuwa ni vema kulipia kodi yako mapema ili kuepuka usumbufu.
LESENI
ZA BIASHARA
Inatozwa
kwa mujibu wa Sheria ya fedha Na.5 ya mwaka 2011. Leseni ambazo zinatozwa na
Halmashauri ni zile za Kundi B. Ili kuondoa urasimu wa upatikanaji wa Fomu za
maombi wafanyabiashara wanaotaka kukata Leseni wanaweza kuzipata fomu hizo
kupitia Tovuti ya Manispaa ya Ilala sehemu ya biashara kwa anuani http://ilala.kpk.fi/@business
au kwa kufika Arnatoglou Chumba NA. 1 ambapo atafahamishwa kiasi cha ada
anachopaswa kulipa.
Baada
ya kulipia ada husika Fomu ya maombi inapaswa kurejeshwa Chumba Na. 5 kwa ajili
ya kuandikiwa leseni ya Biashara.
Baadhi
ya Wafanyabiashara kwa sababu ambazo wanazijua wao wenyewe wamekuwa wakiwatumia
watu wanaojiita Mawakala kwa ajili ya kupata leseni. Kiutaratibu Manispaa haina
wakala wa Leseni za Biashara. Imebainika kuwa, hao mawakala wasio waaminifu
maarufu kwa jina la Vishoka huwapelekea wateja wao leseni feki za biashara za
kughushi ambazo hubainika wakati wa ukaguzi.
Rai
inatolewa kwa Wafanyabishara wote ambao waliwatuma Watu kuwakatia Leseni kufika
katika Ofisi za Manispaa ya Ilala ili
kufanya uhakiki wa leseni zao endapo ni halali au la.
Kuanzia
tarehe 8/04/2015 Manispaa imeanza zoezi la ukusanyaji wa takwimu za majengo na
Leseni za Biashara. Zoezi hili litakalofanyika kwa kipindi cha miezi mitatu lengo
likiwa ni kupata taarifa na takwimu sahihi za wakazi, wamiliki wa majengo ya
biashara na makazi pamoja na wafanyabiashara ndani ya Halmashauri ya Manispaa
ya Ilala. Takwimu hizi zitatumika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wetu.
Aidha linatekelezwa na Maafisa/Watumishi wa Manispaa pamoja na wasaidizi wao
ambao ni vijana wapatao 300 walioajiriwa kwa ajili ya zoezi hili. Maafisa hao
na Wasaidizi hao wanavyo vitambulisho. Kazi
inayofanyika ni kupita katika Mitaa yote kukagua na kuuliza maswali kuhusu
taarifa zinazohusu: Jina kamili la
mmiliki wa jingo la biashara/makazi, Stakabadhi za malipo ya Kodi ya Majengo
yaliyofanyika kwa mara ya mwisho kama zipo na Makadirio ya malipo yaliyofanywa
na Manispaa kama yapo. Inaaminika kuwa baada ya kupata takwimu sahihi Halmashauri itaweza kuboresha takwimu zake na
kuweza kukusanya mapato stahiki kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Manispaa
ya Ilala. Hivyo wafanyabiashara pamoja na Wamiliki wa majengo wanaomba kutoa
ushirikiano ili kufanikisha zoezi hili. Utekelezaji wa zoezi hili ni wa
kisheria hivyo endapo mtu yeyote atashindwa kutoa ushirikiano au kuwakwamisha
Maafisa wanaotekeleza kazi hiyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Imetolewa na,
Ofisi ya Uhusiano
Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala
muweke sehemu ya kudownload sheria ndogo ndogo za halimashauli ya manispaa ya ilala
JibuFuta