Bilioni 2.9 Yatolewa kwa wanufaika wa mikopo ya Asilimia 10% ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii leo Machi 7, 2023 wamefanya hafla ya kukabidhi mikopo kwa vikundi vya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu ambapo shilingi bilioni 2.9 zimetolewa ikiwa ni fedha kwa ajili mkopo wa asilimia 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa wanufaika hao.


Aidha Hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam iliweza kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Wakuu wa Idara, Wadau wa maendeleo kutoka Bank ya CRDB, NMB, DCB, wajasiriamali wanaonufaika na mikopo ya asilimia 10% pamoja na wananchi wengine wa Jiji la Dar es Salaam.


Akizungumza katika hafla iyo DC Mpogolo amesema “Niwaombe sana wanufaika wa mikopo hii muwe na nidhamu ya marejesho ya fedha hizi kwani Mheshimiwa Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatambua uwepo wa makundi haya ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na ndio maana katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mheshimiwa Rais ameweza kuelekeza Halmashauri zote zitoe mikopo kwa makundi haya pia ameruhusu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutoka mkopo hadi bilioni 2.9 lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanajiajiri wenyewe na wanajikwamua kiuchumi hivyo niwaombe mkipewa mikopo hii mhakikishe mnarejesha fedha hizo kwa wakati ili wengine waweze kupata kwani wahitaji bado ni wengi.”


Sambamba na hilo Mhe.Mpogolo ameeleza kuwa japo vikundi hivi vinapata mikopo na vimejiajiri ila Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na timu yake waweze kuwatafutia masoko wananchi hawa wanaopokea mikopo ya asilimia 10%hivyo amewaombaa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia idara yake ya maendeleo ya Jamii wanaandaa Soko angalau mara mbili kwa mwaka kwaajili ya kusaidia vikundi hivi.

Kwa upande mwingine Mhe. Mpogolo amewahakikishia Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Mkurugenzi wa Halmsahauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwa atashirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha wanufaika wa mikopo wanarejesha kwa wakati na kwa wale watakao kaidi watawajibishwa kulingana na kanuni za Kisheria.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Eng. Amani Mafuru ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii inaendelea kutekeleza jukumu la kutenga na kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni fedha kutoka mapato ya ndani ambapo hadi kufikia Juni 2022 takribani shilingi bilion 23.4 ziliweza kutolewa kwa vikundi 1963 vyenye wanufaika elfu 19.8 ambapo shilingi bilioni 19.9 zikiwa ni fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri huku shilingi bilioni 5.5 zikiwa ni fedha kutoka katika marejesho ya mikopo hiyo.

Akiendelea kutoa taarifa katika hafla hiyo Eng.Mafuru amesema “kuanzia mwezi Julai 2023 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeanza kutoa mikopo kwa kuzingatia mfumo wa kielektronic (Ten Percent Loan Management Infomation System) ulioanzishwa na Serikali kuu kwa lengo la kurahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa mikopo hiyo hivyo kupitia mfumo huu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kusajili takribani vikundi 1870 na imepokea jumla ya maombi ya mkopo kwa vikundi 458 vyenye thamani ya shilingi bilioni 33 ambapo baada ya uhakiki Halmashauri imepanga kutoa mikopo hiyo kwa awamu kupitia fedha za marejesho kutoka kwenye mikopo ya vikundi vingine.”


Sambamba na hilo Eng. Mafuru ameeleza kuwa “lkiwa ni awamu ya Kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatoa mikopo kwa vikundi 76 vyenye wanavikundi 360 ambapo vikundi 27 vinatoka Jimbo la Ilala, vikundi 23 kutoka Jimbo la Ukonga huku vikundi 26 vikitoka Jimbo la Segerea ambapo vikundi hivyo vitapewa mkopo kulingana na mgawanyo wa asilimia 4% kwa Wanawake, asilimia 4% kwa vijana na asilimia 2% kwa watu wenye ulemavu kwani vikundi hivi vimeshapata mafunzo na kusaini mikataba tayari kwa kuwekewa hela hizo."

Akitoa Shukurani zake za dhati kwa niaba ys wanavikundi wengine waliopokea hundi za mfano Deogratius Davidi kutoka kikundi cha Good Hope ameweza kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa utoaji wa mikopo bila kusahau juhudi za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuweza kuandaa mafunzo na pia kutoa ushauri kwa vikundi hivyo kwani hii imeweza kupunguza wimbi la ukosekanaji wa ajira kwa vijana hivyo wameahidi kuzitumia fedha hizo kwa umakini na kurejesha marejesho kwa wakati ili wengine waweze kunufaika.Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi