Na David Langa.
Wakazi wa jiji la Dar es salaam wamepongeza juhudi zianazofanywa
na manispaa zote tatu za Ilala, Temeke na Kinononi za kuwaondoa wafanyabiashara
wadogo maarufu kama wamachinga katika maeneo yasiyoruhusiwa. Operesheni hiyo
imesababisha maeneo mengi yaliyokuwa yakitumiwa na wafanyabiashara hao kuwa
wazi na hivyo kuwapa urahisi wa kutembea kati kati ya jiji hasa katika maeneo
ya kariakoo na posta.
Zoezi pia inajumuhisha kuwaondoa omba omba katika makutano
yote ya bara bara hatua iliyokuwa inasababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa
barabara hizo.
Katika manispaa ya Ilala ambayo ndiyo ina sehemu kubwa
inayoathirika na zoezi hili viongozi wakuu wamekuwa wakishiriki moja kwa moja
na wakati wote wa mchana na usiku wakiongozwa na Meya wa Mnispaa hiyo Mh. Jerry Silaa pamoja na Kaimu Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala Dr. Severine Asenga ambao wamekuwa bega kwa bega
kuwaongoza watumishi walio chini yao usiku na mchana.
Shughuli hii inatekelezwa kwa masaa 24 ambapo watumishi na
wakuu wote wa idara wamekuwa wakipeana zamu katika kuwaongoza walinzi na polisi
wanohusika katika zoezi hili maalum kama safisha jiji.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bwana Raymond Mushi na mkuu wa Mkoa
wa Dar Es salaam Bwana Mecky Sadick kwa nyakati tofauti wamewahasa watendaji
wote kuweka mikakati ya kuhakikisha jiji linakuwa safi na kuondoa dhana kuwa ni
zoezi la zima moto.
Wakazi wengi wa jiji wametoa pongezi kwa hatua iliyofikiwa
kwani kuna maeneo ya kati kati ya jiji yalishafanywa soko na hivyo kuwawia
vigumu wapiti kwa miguu na hata waendesha magari.