MADIWANI MANISPAA YA ILALA WAVUTA HISIA ZA WENGI TAMASHA LA PASAKA VISIWANI ZANZIBAR

Na: Hashim Jumbe, kutokea Zanzibar
Timu ya Madiwani wa Manispaa ya Ilala iliyoshiriki tamasha la Pasaka visiwani Zanzibar lililoandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mjini Magharibi imevuta hisia za wapenzi wa michezo visiwani hapa waliojitokeza kwa wingi kuwashuhudia.

Katika mchezo wa ufunguzi wa tamasha hilo uliofanyika katika viwanja vya Amani, timu ya mpira wa miguu ya Madiwani wa Manispaa ya Ilala walipoteza mchezo wao kwa kukubali kufungwa magoli 3-2 na wenyeji wao wa Wilaya ya Mjini Magharibi, licha ya kucheza soka safi na lakuvutia lililowafanya kushangiliwa muda wote wa mchezo.

Aidha, tamasha hilo lilihusisha na michezo mingine mbalimbali iliyochezwa kwenye fukwe za Kizimkazi kama vile michezo ya kuvuta kamba, kukuna nazi, kukimbia na gunia, mbio za ufukweni na kukimbiza kuku.


Katika tamasha hilo ushindi wa jumla umekwenda kwa Manispaa ya Ilala baada ya kufanya vyema kwenye mashindano ya ufukweni na kupata kikombe na medali za shaba huku Mheshimiwa Tumike aking’ara kwenye shindano la kukuna nazi, Mheshimiwa Mtumwa Mohamed akishika nafasi ya kwanza kwa kukimbia na gunia.


Timu ya Madiwani wa Manispaa ya Ilala waliovaa jezi za kijani wakiwa kwenye picha ya pamoja na timu ya Madiwani wa Wilaya ya Mjini Magharibi wakati wa mchezo wa ufunguzi wa tamasha la pasaka uliofanyika kwenye uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.



Madiwani Wanawake wa Manispaa ya Ilala wakiongozwa na Hajjat Lai Ninga wakishiriki shindano la kuvuta kamba kwenye tamasha la Pasaka visiwani Zanzibar

Diwani wa Kata ya Tabata(kulia) Mh. Mtumwa Mohamed akiongoza mbio za kukimbia na gunia kwa Madiwani Wanawake







Diwani wa kata ya Ilala Mh. Edson Fungo akikuna nazi katika shindano la kumtafuta mshindi wa kukuna katika fukwe za Kizimkazi


Wakati huohuo Madiwani wa Manispaa ya Ilala wametumia tamasha hilo la Pasaka kuagana na Madiwani wenzao wa Wilaya ya Mjini Magharibi na Kuombeana kila la kheri katika uchaguzi Mkuu ujao na kupeana zawadi mbalimbali ikiwa ni ishara ya kudumisha umoja wa Ilala-Magharibi




Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii Manispaa ya Ilala, Mh. Angelina Malembeka akimkabidhi kalenda za Manispaa ya Ilala Mwenyekiti wa Wilaya ya Mjini Magharibi



1 Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi