Na:
Hashim Jumbe
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kupitia kikao chake cha kawaida limepokea,
limejadili na kupitisha taarifa za utendaji kazi kutoka Kata zote 36 zilizopo
Manispaa ya Ilala kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba kwa mwaka huu wa
2016.
Taarifa hizo za utendaji kazi zimewasilishwa na
Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo kutoka kwenye kila Kata, ambapo Baraza la Madiwani
walizipokea, kuzijadili na kuzipitisha taarifa zote kutoka kwenye Kata 36.
Kata hizo ni pamoja na Buyuni, Zingiziwa, Kitunda,
Majohe, Kariakoo, Kiwalani, Kimanga, Upanga Magharibi, Mnyamani, Upanga
Mashariki, Mchafukoge, Kivule, Mzinga, Tabata, Kipawa, Kivukoni, Liwiti,
Kinyerezi, Msongola, Minazi Mirefu, Kisukuru, Gerezani, Kisutu, Segerea,
Chanika, Mchikichini, Buguruni, Pugu, Ilala, Vingunguti, Bonyokwa, Jangwani, Gongolamboto,
Pugu Stesheni, Ukonga na Kipunguni.
Wakati wa uwasilishwaji wa taarifa hizo za kazi, taarifa ya Kata ya Kariakoo iliyowasilishwa na Mhe. Abdulkarim Masamaki iliibua mjadala mzito kutoka kwa Wajumbe wa Kikao hicho ambapo walitaka wapatiwe ufafanuzi wa zoezi la kuwaondoa Wamachinga maeneo ya katikati ya mji na kuwaelekeza kata za pembezoni mwa mji.
Hoja hiyo ilitolewa ufafanuzi na Katibu Tawala wa Wilaya
ya Ilala, Ndugu Edward Mpogolo ambapo alisema “teyari maeneo ya kuwapeleka
yameshatengwa kama alivyoelekeza Mhe. Rais katika hotuba yake aliyoitoa kwenye
viwanja vya Furahisha-Mwanza, kuwa yafanyike mazungumzo na Wamachinga na
mkishakubaliana muone mtakapo watengea maeneo rafiki ya kufanyia biashara zao,
ikiwemo miundombinu ya vyoo, umeme na kituo cha daladala, kwa maana hiyo
tumewaelekeza kwenye soko la Kivule na Kigogo fresh ambapo teyari miundombinu
imeshakamilika”
Kufuatia hatua hiyo, Mwenyekiti wa kikao hicho
Mstahiki Meya Charles Kuyeko aliunda kamati ya Wajumbe Watatu kufuatilia mpango
huo wa kuwahamisha Wamachinga maeneo ya katikati ya Mji na kuwapeleka kata za
pembezoni na kuona namna iliyo bora ya kuendesha gulio kuanzia siku ya Ijumaa
mchana, Jumamosi na Jumapili iwe kwa siku nzima, ambapo itakuwa inafungwa mitaa
ya Lumumba na Mkunguni.
|
Mstahiki Meya Manispaa ya Ilala, Mhe. Charles
Kuyeko akiongoza sala ya kuombea Kikao cha Baraza la Madiwani na Taifa kwa
ujumla |
|
Madiwani kutoka Kata mbalimbali za Manispaa ya
Ilala wakifuatilia mijadala iliyokuwa ikiendelea kwenye Kikao cha Baraza la
Madiwani |
|
Diwani wa Kata ya Kitunda, Mhe. Nice Gisunte akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi Kata ya
Kitunda kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka 2016. |
|
Katibu Tawala Wilaya Ilala, Ndugu Edward Mpogolo
akitoa ufafanuzi wa hoja iliyojitokeza wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Kata ya
Kariakoo, hoja ya kuwaondoa Wamachinga maeneo ya katikati ya Mji na kuwapekeka
maeneo ya pembezoni mwa Mji ikiwemo Kata ya Kivule yenye Soko la Kivule na
sokola Kigogo fresh lilipo Kata ya Pugu.
|
|
Waandishi wa Mikutano wakiendelea kuchukua
kumbukumbu za Kikao wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani, Kikao maalum cha
kupokea na kupitisha taarifa za Kata kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka
2016 |
|
Wakuu wa Idara mbalimbali za Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala wakifuatilia kikao cha Baraza la Madiwani |
|
Diwani wa Kata ya Upanga Mashariki, Mhe. Sultan
Salim akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi ya Kata ya Upanga Mashariki kwa
kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka 2016. |