Vikundi vya Ukusanyaji, Uchakataji na Urejelezaji taka vyapokea vifaa ya usafi

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira kwa kushirikiana na Taasisi za Mazingira Plus na TACSS kwa ufadhili wa umoja wa Majiji duniani (C40 Cities) leo Juni 19, 2024 wamekabidhi vifaa kwa wanufaika wa mradi Jumuishi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hafla iliyofanyika katika Ofisi za Kata ya Vingunguti Jijini humo.


Akiongea wakati wa hafla hiyo, Afisa Mazingira wa Jiji la Dar es Salaam ambaye ni Mratibu wa mradi huo Bi. Monica Mosha amesema “Mradi Jumuishi wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi umeanza kutekelezwa Oktoba 2023 na unatarajiwa kukamilika Juni 2024 ukiwa umelenga kusaidia uendelezaji wa njia bora na endelevu za kuthibiti taka oza (Organic Waste) pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa Afya kusaidia uanzishwaji wa njia ya udhibiti wa taka oza kupitia vikundi vya Jamii na wabeba taka ambapo kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam mradi huu tumeutekeleza katika Kata ya Vingunguti kwani kutokana na ufinyu wa maeneo magari ya Taka hushindwa kupita hivyo taka nyingi hutupwa mto msimbazi na ndio maana tukatekeleza mradi huu Kata ya Vingunguti ili kuzuia utupaji taka Mto Msimbazi.”


Sambamba na hilo, Bi. Mosha ameendelea kusema “vifaa vinavyotolewa kwa vikundi vya kukusanya, kuchakata na kurejeleza taka ni pamoja na gum boots 60, Reki 10, Chepeo 10, fork spade 10, mizani 10, Gloves 20, toroli 10, mikokoteni 10, viroba 6000, reflector 120, overall 20, ujenzi wa kituo cha kupokelea taka rejelezi chenye jumla ya chemba 5, sehemu za kuzalishia chakula cha kuku chenye jumla ya chemba 4, kifaa cha kuchakata majani, chekecheke za mboji 4 pamoja na eco-bins 3 ambapo kupitia vifaa hivi tunaamini mazingira yetu yatakua katika hali ya usafi na tutaepukana na magonjwa ya mlipuko hivyo niwaombe mvitumie vifaa hivyo kwa utunzaji ili viweze kudumu kwa muda mrefu.”


Akitoa Shukrani zake kwa Niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Meneja wa Kanda namba 3 Bw. Kefa Dan Gembe ameeleza kuwa Mradi huu ni muhimu kwani utaleta matokeo chanya katika utunzaji wa mazingira na afya za wananchi wa Jiji la Dar es Salaam hususani wananchi wa Vingunguti huku akihakikisha kusimamia na kuendesha mradi huu kwa ufanisi mkubwa kwa lengo la kuendelea kupendezesha Jiji na kulinda afya za wanajamii.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi